Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Namuelewa vizuri Denis Kitambi

Denis Kitambi 1080x640 Namuelewa vizuri Denis Kitambi

Fri, 15 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Namungo FC haikuwa na mwanzo mzuri katika Ligi Kuu ya NBC msimu huu, jambo lililopelekea kutimuliwa kwa kocha Cedrick Kaze.

Baada ya kuchukua uamuzi huo wa kumtimua Kaze, uongozi wa Namungo FC ukaamua kutoajiri kocha mpya na badala yake jukumu la ukocha mkuu akapewa msaidizi wake Denis Kitambi ambaye ana vigezo kikanuni vya kuhudumu katika nafasi hiyo.

Mchezo wa kwanza tu akiwa kocha mkuu, Kitambi akaiongoza Namungo FC kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 ugenini dhidi ya Azam FC kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

Hata hivyo, ushindi huo haukutosha kutupa imani wengi kwamba Kitambi amejipata ndani ya Namungo FC kwa sababu imetokea mara nyingi kocha mpya anapoingia kweye timu, inaanza kwa kupata ushindi au sare kama ilikuwa na mwenendo mbovu kwani wachezaji wanakuwa na hamu ya kumuonyesha kocha kuwa wanastahili nafasi chini yake.

Mechi kama tano hivi kwa kocha mpya ndio zinaweza kutumika kutoa tathmini kama kocha yuko vizuri au alipata matokeo ya kuvutia mwanzoni kwa hamasa tu hivyo kwa Kitambi akatuthibitishia kwamba hakubahatisha.

Katika mechi zake sita za mwanzo, akapata ushindi mara tatu, akatoka sare mbili na kapoteza mchezo mmoja hivyo sio suala la morali ni juhudi zake kwa kushirikiana na benchi la ufundi.

Hata namna wachezaji wa Namungo FC wanavyocheza unawaona wazi kuwa wanafurahia kile wanachofundishwa na kupewa na kocha Kitambi jambo ambalo linawafanya wapate matokeo kwa urahisi katika mechi zao chini yake.

Nilitegemea kuona Kitambi angebaki na Namungo hadi mwisho mwa msimu ili aisaidie zaidi timu hiyo kufanya vizuri kwenye ligi na kuzidi kuimarisha wasifu wake lakini ghafla taarifa imetolewa kuwa ameachana na timu hiyo na inaripotiwa kwamba anaenda Geita Gold.

Geita hapana shaka anaenda kukutana na presha kubwa kwa vile timu ipo katika nafasi mbaya kwenye msimamo wa ligi na ni kama anaenda kuanza upya.

Chanzo: Mwanaspoti