Ligi Kuu Bara imesimama kupisha kalenda ya Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) inayohusisha mechi za timu za taifa.
Ligi hiyo imesimama wakati ambao baadhi ya timu zimecheza mechi 21, nyingine 20 na Simba ikiwa ndiyo iliyocheza chache - 19.
Kwa hesabu za kawaida, ligi hiyo yenye timu 16 kuna timu zimebakiza mechi 10, nyingine tisa na Simba imebakiza 11 ili kumaliza msimu. Mwanaspoti kupitia makala linakuletea takwimu (data) za Ligi Kuu Bara hadi iliposimama baada ya mechi ya Azam na Yanga Jumapili.
UBINGWA Mbio za ubingwa hadi sasa zinaonekana kusalia kwa timu tatu za Yanga, Simba na Azam.
Yanga ndiyo inaongoza ligi na alama 52 baada ya mechi 20 ikifuatiwa na Azam yenye 47 baada ya mechi 21 kisha Simba pointi 45 baada ya mechi 19.
Timu moja kati ya hizo tatu itakayochanga vyema karata zake kwenye mechi zilizobaki itaibuka bingwa, lakini hadi sasa Yanga ina nafasi kubwa ya kuzishinda Simba na Azam.
TOP FOUR Ha-di sasa, Tanzania ina tiketi ya kupeleka timu nne kwenye mashindano ya CAF msimu ujao na hilo limefanya vita ya kuwania nafasi nne za juu kuwa kali. Yanga, Azam na Simba zina nafasi kubwa ya kukaa hapo, lakini vita ipo kwenye timu moja itakayoingia kukaa mezani na vigogo hao.
Coastal Union ipo nafasi ya nne na alama 30 lakini chini yake zipo Tanzania Prisons na KMC zenye alama 28 kila moja.
Singida Fountain Gate na Kagera Sugar nazo haziko mbali kwani zina alama 24 hivyo yoyote inaweza kupanda katika mechi tisa zilizobaki.
Hapo kuna vita kali ambayo timu mojawapo kati ya hizo inaweza kushinda na kuungana na Simba, Azam na Yanga kimataifa msimu ujao.
KUSHUKA DARAJA
Huko nako vita ni kali. Timu zinapambana kutoshuka daraja. Mtibwa Sugar ipo mkiani na alama 16 baada ya mechi 20. Juu yake ipo JKT iliyovuna pointi 20 kwenye mechi 20, nafasi za 12, 13 na 14 zipo Mashujaa, Tabora United na Geita Gold kila moja ikiwa na alama 21 baada ya mechi 21, tofauti ikiwa ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Ukiachana na hizo zilizopo chini vita hiyo bado nzito kwa kila timu kwani yoyote itakayoteleza kwenye mechi zilizobaki inaweza kushuka daraja. Ikumbukwe msimu huu zinashuka daraja timu mbili moja kwa moja, huku nyingine mbili zikicheza mechi za mtoano kuwania kusalia Ligi Kuu.
MABAO Hadi sasa yamefungwa jumla ya mabao 346 kwenye ligi ambapo Yanga inaongoza ikiwa imefunga 49 ikifuatiwa na Azam iliyofunga 47 kisha Simba iliyofunga 39 huku Kagera Sugar ikiwa timu iliyofunga mabao machache zaidi, ikicheka na nyavu mara 13 tu.
Mtibwa Sugar ndiyo timu iliyofungwa mabao mengi zaidi, 34 ikifuatiwa na KMC iliyoruhusu 31, kisha Ihefu iliyopachikwa 29 huku Yanga ikiwa timu iliyoruhusu mabao machache zaidi, 11.
Kinara wa upachikaji mabao ni viungo wa Yanga, Stephane Aziz Ki na Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam wote wakifunga mabao 13, kisha Wazir Junior wa KMC aliyecheka na nyavu mara 11.
ASISTI Winga wa Azam, Kipre JR ndiye anaongoza kwa pasi za mwisho ‘asist’ akiwa nazo nane, akifuatiwa na Kouassi Attohoula na Stephene Aziz Ki wenye saba kila mmoja.
Fei Toto, Impiri Mbombo wa Tabora United, Rahim Shomari na Awesu Awesu wa KMC, na Clatous Chama kila mmoja anazo nne.
KADI Hadi sasa zimetoka kadi za njano 529 ambapo Singida Fountain Gate na Dodoma Jiji ndizo zinaongoza kila moja ikiwa imepata kadi 46, zikifuatiwa na Ihefu yenye kadi 41.
Simba ndiyo timu iliyoonyeshwa kadi chache za njano hadi sasa ikipata 17. Wema Sadoki wa JKT ndiye mchezaji anayeongoza kwa kupata kadi za njano akiwa nazo nane akifuatiwa na Greyson Gerald wa Coastal Union na Andy Lobuka wa Tabora United wenye nazo sita.
Kadi nyekundu zimetoka 18 kwa wachezaji tofauti wa timu 12 za ligi ambapo Singida Fountain Gate inaongoza ikiwa imekula umeme mara mbili, ikifuatiwa na Namungo, Kagera Sugar, Tanzania Prisons na Dodoma Jiji ambazo kila moja imepata umeme mara mbili.
Simba, Azam, Mtibwa Sugar na Tabora United ndizo hazijapata kadi nyekundu. Pia hakuna mchezaji aliyepata kadi nyekundu mara mbili.
CLEAN SHEETS Yanga ndiyo inaongoza kwa kutoruhusu bao kwenye mechi ‘clean sheets’ ikiwa imefanya hivyo mara 13 ikifuatiwa na Coastal Union iliyofanya hivyo mara 11 kisha Azam na Geita Gold zilizofanya hivyo mara tisa kila moja huku Mtibwa Sugar ikiwa ndiyo timu yenye wastani wa mkubwa wa kuruhusu nyavu zake kutikisika kwenye mechi ambapo ni mechi tatu ambazo timu hiyo ilitoka bila kipa kuokota mpira nyavuni.
Kipa wa Coastal Union, Ley Matampi ndiye kinara wa clean sheet akiwa nazo 10 akifuatiwa na Djigui Diarra wa Yanga mwenye nane kisha John Noble wa Tabora na Costantine Deusdedith wa Geita wenye saba kila mmoja.