Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Namba zimewakataa kabisa Ligi Kuu Bara

Morrison Aziz Ki  . Morrison na Aziz Ki

Fri, 21 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Zumebaki raundi nne kabla ya kumalizika kwa Ligi Kuu msimu huu ambapo Yanga inaongoza msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 68 ikifuatiwa na Simba yenye pointi 63, huku Singida Big Star yenyewe ikiwa nafasi ya tatu na pointi zake 51.

Wakati ligi ikielekea ukingoni, zipo timu, wachezaji ama makocha ambao takwimu zinaonekana kutowaweka katika nafasi nzuri ya kutimiza malengo fulani na hivyo baadhi watahitajika kufanya kazi ya ziada katika mechi nne zinazofuata.

Wapo ambao namba zimewakataa kushindwa kuvunja au kufikia rekodi fulani, kuna ambao zinawaweka katika nafasi ngumu kulingana na msimamo na ratiba ya ligi ilivyo na wapo wengine ambao zimekuwa tofauti nao katika suala la hatima zao kwenye klabu walizopo siku za usoni.

POLISI TANZANIA KUBAKI LIGI KUU (19) Maafande wa Polisi Tanzania wako mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu wakiwa na pointi 19 ambazo ni saba (7) pungufu ya zile za KMC iliyo katika nafasi ya 14.

Ili waepuke kushuka daraja moja kwa moja, Polisi Tanzania wanapaswa kupata ushindi katika mechi zao zote nne zilizobakia dhidi ya Ihefu SC na Mtibwa Sugar nyumbani na pia dhidi ya Simba na Azam ugenini na kisha kuziombea mabaya KMC, Mbeya City, Coastal Union, Dodoma Jiji, Tanzania Prisons na Mtibwa Sugar zipoteze mechi zao zote zilizosalia ili yenyewe iweze kunusurika.

Kwa nafasi waliyopo na mechi walizobakiza, mazingira hayaonekani kuwapa nafasi kubakia kwenye ligi.

SINGIDA BIG STARS KUMALIZA NAFASI YA PILI Kitendo cha Simba kuibuka na ushindi dhidi ya Yanga, Jumapili iliyopita kimeiweka Singida Big Stars katika mazingira magumu ya kumaliza ligi katika nafasi ya pili kwenye msimamo na inategemea miujiza ili hilo liweze kutokea.

Kwa sasa Singida Big Stars yenye pointi 51, imezidiwa kwa pointi 12 na Simba na ili iweze kumaliza katika nafasi ya pili, inahitajika kupata ushindi katika mechi zake zote nne zilizobakia dhidi ya Yanga, KMC, Namungo na Ruvu Shooting tena kwa idadi kubwa ya mabao na kisha kuombea Simba ipoteze mechi zake zote ambazo imebaki nazo dhidi ya Namungo, Coastal Union, Polisi Tanzania na Ruvu Shooting.

YANGA KUVUNJA REKODI YA SIMBA Simba ndio timu inayoshikilia rekodi ya kuwa timu iliyowahi kukusanya idadi kubwa ya pointi katika msimu mmoja ambapo ilikusanya pointi 93 katika msimu wa Ligi Kuu 2018/2019.

Kwa hali ilivyo, hakuna uwezekano kwa Yanga inayoongoza ligi msimu huu kuivunja rekodi hiyo ya Simba kwani ikipata ushindi katika mechi zake zote nne zilizobaki dhidi ya Singida Big Stars, Dodoma Jiji, Mbeya City na Tanzania Prisons, itafikisha pointi 80 tu.

SIMBA NA REKODI YA TOFAUTI YA MABAO Katika msimu wa 2018/2019, Simba iliweka rekodi ya kumaliza ikiwa na utofauti mkubwa zaidi wa mabao ya kufunga na kufunga ambapo ilimaliza ikiwa nayo 62, ikifunga mabao 77 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 15.

Wakati ikibakiza mechi nne kumaliza msimu huu, hadi sasa utofauti wa mabao ya kufunga na kufungwa ya Simba ni 48 na hivyo ili ivunje rekodi yake iliyojiwekea msimu wa 2018/2019, inapaswa kuhakikisha inafunga 14 au zaidi ya hapo ikiwa itaruhusu nyavu zake pia zitikisike.

MAYELE NA KIGINGI CHA MMACHINGA Rekodi ya mchezaji aliyefunga idadi kubwa ya mabao katika msimu mmoja wa Ligi Kuu Tanzania Bara, inashikiliwa na Mohammed Hussein 'Mmachinga' aliyepachika mabao 26 katika msimu wa mwaka 1999 akiwa na kikosi cha Yanga.

Mwanzo mzuri wa Fiston Mayele, katika ufungaji msimu huu uliwafanya wengi waamini kuwa ataivunja au kuifikia rekodi hiyo lakini wakati Yanga ikibakiza mechi nne, mshambuliaji huyo anapaswa kufunga mabao tisa ili aifikie rekodi ya Mmachinga na ili aivunje anatakiwa kufunga mabao 10 katika mechi zilizobaki.

KMC KURUDIA YA MSIMU ULIOPITA Ilionekana msimu wa 2020/2021, KMC ilikusanya pointi ndogo zadi katika Ligi tangu ipande daraja ambapo ulipomalizika ilikuwa na pointi 46.

Hata hivyo msimu huu unaonekana kuwa mgumu zaidi na hakuna uwezekano wa timu hiyo kuzifikia au kukusanya idadi kubwa ya pointi kulinganisha na msimu huo kwani hadi sasa inazo 26 na hata ikiongeza 12 zilizobaki katika mechi nne za mwisho itakuwa na pointi 38 na hivyo kuufanya huu kuwa msimu mbaya zaidi katika historia ya KMC.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: