Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Namba zawaondoa Phiri, Moloko

Ducapel Molokoo Jesus Moloko

Wed, 17 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Uamuzi mgumu wa Simba kuachana na mshambuliaji Moses Phiri na Yanga kuachana na winga Jesus Moloko jana unaonekana kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na kiwango kisichoridhisha ambacho wawili hao wamekuwa nacho msimu.

Licha ya wawili hao kila mmoja kuwa na mwanzo mzuri katika kikosi cha timu yake baada ya kusajiliwa, mambo yameonekana kuwabadilikia msimu huu ambapo wamekuwa na namba ndogo ya mabao waliyohusika nayo katika mashindano tofauti waliyoshiriki jambo lililoshawishi makocha Abdelhak Benchikha wa Simba na Miguel Gamondi wa Yanga kushauri wapigwe panga ili kupisha nyota wapya.

Kwa upande wa Simba, Phiri amefungua milango ya kuingia kwa mshambuliaji Omar Jobe wakati Jesus Moloko kwa Yanga kuondoka kwake kumetoa nafasi kwa Augustine Okrah.

Katika Ligi Kuu ya NBC msimu huu, Phiri amecheza dakika 278 katika mechi tisa ikiwa ni wastani wa dakika 31 kwa mchezo, huku akifunga mabao matatu tu wakati Moloko amecheza mechi sita kwa dakika 334 sawa na wastani wa dakika 55 pasipo kufunga bao lolote, akipiga pasi mbili tu za mwisho.

Yanga jana ilitangaza rasmi kuachana na Moloko ingawa watani wao Simba hawakufanya hivyo kwa Phiri japo habari za uhakika ambazo gazeti hili linazo ni kuwa pande hizo mbili zimefikia makubaliano ya kuvunja mkataba baina yao.

"Young Africans SC tumefikia makubaliano ya pande zote mbili kusitisha mkataba na mchezaji Jesus Ducapel Moloko.," ilifafanua taarifa ya Yanga.

Mbali na Moloko, Yanga pia ilikuwa mbioni kuachana na Hafidh Konkoni ambaye alitarajiwa kupisha usajili wa mshambuliaji mpya ndani ya timun hiyo.

Kwa upande wa Simba, hadi wakati gazeti hili linakwenda mitamboni, ilikuwa katika kikao cha kufanya uamuzi wa mwisho wa kati ya Clatous Chama au Aubin Kramo nani aondoke kupisha usajili wa Boubacar Sarr ambaye naye amenaswa katika dirisha hili dogo.

Kipa wa Singida Fountain Gate, Beno Kakolanya alisema Phiri ameponzwa na majeraha.

"Phiri ni kama alitoka mchezoni, ila ni straika anayejua kufunga na kuna siku bosi mmoja wa Simba niliwahi kumshauri wasiachane naye, msimu uliyopita asingeumia binafsi angeibuka mfungaji bora," alisema Kakolanya.

Staa wa zamani wa Yanga Sekilojo Chambua alisema, "Moloko mwaka jana alikuwa kwenye kiwango cha juu na msimu huu kashuka, ila kuhusu Konkoni kastahili kuondoka kwani kapewa nafasi ya kutosha alikuwa hafungi."

Chanzo: Mwanaspoti