Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Namba za Yanga zaanza kutisha Ligi Kuu

Pacomeeeeeee Namba za Yanga zaanza kutisha Ligi Kuu

Sat, 17 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ile furaha iliyozoeleka kwa mashabiki wa Yanga imerudi tena baada ya timu hiyo kurejesha zile dozi katika Ligi Kuu Bara kwa kuifumua KMC mabao 3-0 kwenye pambano lililopigwa Uwanja wa Jamhuri Morogoro ikishuhudiwa kipa Djigui Diarra akirejea langoni tangu atoke kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023.

Hata hivyo, kufuatia ushindi huo namba za alama ilizokusanya Yanga hadi sasa ambazo ni 43 ni kama zimeanza kutishia wapinzani wake kwani inaizidi Simba inayoshika nafasi ya pili kwa pointi saba wakiwa na alama 36, ambayo ni sawa na michezo mitatu.

Katika mechi nne zilizopita za Yanga tangu kurejea kwa ligi baada ya mapumziko ya kupisha Kombe la Mapinduzi 2024 na Afcon iliyofanyika Ivory Coast, ilikuwa ikitaabika mbele ya wapinzani licha ya kushinda mara tatu na kulazimishwa suluhu na Kagera Sugar, lakini imewapa burudani mashabiki.

Ikiwa imekamilika kuanzia langoni hadi eneo la mbele ambalo Maxi Nzengeli, Stephane Aziz KI na Pacome Zouzoua walianza sambamba na Mudathir Yahya waliupiga mwingi na kuizima KMC, licha ya kuwa wenyeji wa mchezo huo.

Mudathir Yahya ameendeleza moto kwa kufunga mabao mawili, huku Pacome akiongeza la tatu na kuwafanya nyota hao wawili kila mmoja kufikisha mabao sita msimu huu, lakini kikiwa kipigo cha pili mfululizo kwa KMC mbele ya Yanga msimu huu baada ya 5-0 kwenye mechi ya duru la kwanza pale Azam Complex.

Ushindi huo umeifanya Yanga kuzidi kuweka hai matumaini ya kutetea ubingwa kwa msimu wa tatu mfululizo ikifikisha pointi 43 baada ya mechi 16, huku ikikusanya mabao 39 na kufungwa manane, ilihali KMC ikisalia nafasi ya tano ikiwa na pointi 22 kupitia michezo 16.

Hicho kilikuwa kipigo cha tisa kwa KMC mbele ya Yanga katika mechi 11 zilizokutana kwenye ligi tangu ilipopanda daraja msimu wa 2018-2019, huku ikishinda mara moja na michezo miwili ikimalizika kwa sare, ikiruhusu pia mabao 21 na kufunga matano.

MCHEZO ULIVYOKUWA

Yanga imeanza kwa kasi na kuandika bao la kwanza sekunde chache baada ya kipyenga cha mwamuzi Omari Mdoe likiwekwa kimiani naMudathri Yahya akitumia makosa ya kipa wa KMC, Wilbol Maseke aliyekuwa anaondoa mpira kisha kunaswa na Yanga ambapo ikatokea piga nikupige na kiungo mshambuliaji huyo kuunasa mpira na kuujaza wavuni na hadi dakika 45 zinamalizika vinara hao walikuwa mbele kwa bao 1-0.

YANGA INAKABA

KMC italazimika kurudi darasani chini ya kocha Abdihamid Moalin kuvumbua mtego wa Yanga kwani mapema tu wachezaji wake walionekana kushindwa kuhimili presha ya wageni wao wanapokuwa wanautafuta mpira na kujikuta wanapoteza kirahisi.

Wenyeji walipiga mashuti mawili yaliyolenga lango dakika ya 45 za kwanza huku moja pekee la beki Rahim Shomari kwa mpira wa adhabu ndogo ndio lililokuwa hatari, kipa wa Yanga Diarra akipangua kiufundi na kuwa kona.

KMC imeshindwa kuupenya ukuta wa Yanga uliokuwa chini ya Diarra na mabeki Yao Kouassi, Nickson Kibabage, Ibrahim Bacca na Dickson Job wakipigwa tafu na Khalid Aucho.

MASEKE/ELIAS WAZICHAPA

Katika tukio lililoshangaza wengi dakika ya 42 kipa wa KMC, Maseke alimtupia ngumi kiungo wake Ibrahim Elias huku naye akijibu mapigo kabla ya wenzao kuwaamulia.

Tukio hilo limetokea wakati kipa huyo aliyeonekana kutokuwa sawa akiwa na makosa mengi kufanya kosa lingine ambapo Elias alipokwenda kuongea naye akajikuta anaambulia konde.

Mwamuzi Mdoe kutoka Tanga alitoa kali akishindwa kutoa kadi kwa wawili hao, ingawa baadaye kabla ya kuanza kwa kipindi cha pili KMC ilimtoa Maseke na kuingia Denis Richard.

GUEDE ANAJITAFUTA

Mashabiki wa Yanga wataendelea kusubiri kuona bao la kwanza la mshambuliaji mpya Joseph Guede ambaye jana aliingia dakika ya 45 ya kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Mzize, lakini akakosa bahati ya kuweka mpira wavuni.

Guede ametengeneza nafasi mbili za wazi, moja ya kichwa ikigonga mwamba huku lingine kipa Richard akipangua na kuwa kona.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: