Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Namba hazidanganyi! Messi vs Ronaldo kuna mtu kafunikwa

Namba Pic Lionel Messi na Cristiano Ronaldo

Tue, 6 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Mkali Lionel Messi amesherehekea mechi yake ya 1,000 kwa staili ya kipekee kabisa, Ijumaa iliyopita.

Mechi ya mtoano hatua ya 16 bora kwenye Kombe la Dunia 2022 huko Qatar kati ya Argentina na Australia, ilikuwa mechi ya 1,000 kwa Messi kuwapo ndani ya uwanja kwa timu yake ya klabu na timu yake ya taifa katika soka.

Katika mechi hizo, Messi aliitumikia mara 778 Barcelona, mechi 169 akiwa na kikosi cha Argentina na mara 53 ameitumikia Paris Saint-Germain, kufanya jumla ya mechi 1,000.

Na mkali huyo mwenye umri wa miaka 35, alisherehekea kufikisha mechi 1000 kwa staili ya kipekee, akifunga bao kwenye mechi ya mtoano ya Kombe la Dunia, ikiwa ni mara yake ya kwanza kwenye maisha yake ya soka, hivyo kuisaidia Argentina kushinda mabao 2-1 mbele ya Australia na kutinga hatua ya robo fainali katika fainali hizo za Qatar.

Baada ya Messi kufikisha mechi 1000, ukaibuka mjadala wa kumhusu supastaa Cristiano Ronaldo, ilikuwaje alipofikisha idadi kama hiyo ya mechi. Wanafanana vipi, namba zao zikoje baada ya mechi 1,000?

Ukweli ni kwamba kwa Messi kufikisha idadi ya mechi 1,000 ni kitu kigumu kuacha kumlinganisha na Ronaldo. Supastaa Ronaldo ni mkubwa kwa miaka miwili kwa Messi, naye alifikisha mechi 1,000 kwenye mchezo wa soka.

Je, takwimu za Messi zikoje kwenye mechi hizo 1,000 ukilinganisha na alivyofanya Ronaldo? Na hapo ndipo unapoibuka mjadala mwingine wa nani zaidi baina ya Messi na Ronaldo. Nani mwenye namba bora kabisa baina yao wawili katika mechi zao 1,000 kwenye maisha yao ya soka. Ronaldo alisherehekea mechi zake 1,000 kwa kuifunga SPAL wakati huo akiitumikia Juventus, Februari 2020. Messi amesherehekea kwa kuifunga Australia kwenye mtoano wa Kombe la Dunia.

Nani mshindi? Jibu utatoa mwenyewe, kitu ambacho Mwanaspoti itajaribu kukiweka hapa ni takwimu za wachezaji hao, chaguo litabaki kuwa kwako ni nani zaidi kati ya Messi na Ronaldo katika mechi zao 1,000.

Kwa kukurahisishia tu, Ronaldo namba zake ni chache kwenye mabao, asisti, mabao yasiyokuwa ya penalti, mataji, Ballon d’Or na Kiatu cha Dhahabu cha Ulaya, huku eneo analomzidi Messi ni kwenye mabao ya kimataifa tu, ambapo katika mechi hizo 1,000 za kwanza, Ronaldo amemzidi mpinzani wake huyo kwa tofauti ya mabao matano. Messi amefunika kwa kufunga mabao mengi yasiyokuwa ya penalti licha ya kucheza mechi chache dhidi ya mpinzani wake, mechi 143.

Chanzo: Mwanaspoti