Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nafasi nyingine kwa timu za Zenji

GCmgIHcXcAAI DZ.jpeg Wachezaji wa Mlandege

Tue, 2 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Msimu wa 18 wa michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024 unaendelea kushika kasi visiwani Zanzibar kwa klabu 12 kutoka mataifa matano yakichuana kuwania taji la msimu huu.

Kwa muda wa siku 17 klabu hizo zitakuwa bize kuchuana kuandika rekodi ya kubeba ubingwa unaoenda sambamba na miaka 60 ya Mapinduzi Zanzibar yaliyofanyika Januari 12, 1964 siku chache baada ya visiwa vya Zanzibar kupata Uhuru Desemba 10, 1963.

Klabu shiriki za msimu huu ni nne kutoka Tanzania Bara, Simba, Yanga, Azam FC na Singida Fountain Gate, timu tano za Zanzibar, wakiwamo watetezi, Mlandege, JKU, Chipukizi na Jamhuri zinazotoka visiwa vya Unguja na Pemba na nyingine tatu za kigeni, Vital'O ya Burundi, Jamus ya Sudan Kusini na APR ya Rwanda zinazoshiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza tangu michuano ilipoasisiwa mwaka 2007.

Timu hizo zimepangwa kwenye makundi matatu yenye timu nne kila mmoja, Kundi A likiwa na Mlandege, Azam, Vital'O na Chipukizi, wakati Kundi B lina Simba, Singida, JKU na APR, huku Kundi C lina timu za Yanga, Jamus, Jamhuri na KVZ.

Mwanaspoti linaiangalia michuano ya msimu huu na mtihani ilizonazo klabu za Zanzibar mbele ya timu nyingine shiriki katika kusaka ubingwa wa Kombe la Mapinduzi 2024 ili kunogesha sherehe za Miaka 60 ya Mapinduzi itakayoadhimishwa siku moja kabla ya fainali itakayopigwa Januari 13.

ISHU IPO HIVI

Licha ya ukweli michuano ya Kombe la Mapinduzi kufanyika Zanzibar na kuzifanya timu za visiwani hivyo kuwa ndio wenyeji, lakini kwa miaka 17 iliyopita ni mara mbili tu, timu hizo zimebeba ubingwa.

Moja ni mwaka 2009 zilipokutana timu za visiwani humo na pili msimu uliopita ambapo Mlandege iliizima Singida na kubeba taji lililokuwa la pili kwa klabu za visiwa hivyo.

Fainali ya kwanza na pekee iliyokutanisha timu za Zanzibar tupu ilipigwa katika msimu wa tatu wa michuano hiyo yaani mwaka 2009 wakati Miembeni ilipowazamisha mabaharia wa KMKM kwa bao 1-0.

Baada ya fainali hiyo, timu za visiwani zilifika fainali nyingine tatu tu, mbili zikipoteza na moja ambayo ni ya msimu uliopita ndipo timu ya Zenji ilijitutumua na kubeba ubingwa.

Ilianza Ocean View iliyocheza fainali na Mtibwa Sugar mwaka 2010, lakini timu hiyo iliyojipatia umaarufu mkubwa mara ilipoibuka, ilipoteza kwa kulala kwa bao 1-0 lililowekwa kimiani na kocha mkuu wa sasa wa Mtibwa Sugar, Zubeiry Katwila enzi hizo akiupiga kama kiungo akitupia bao hilo katika dakika ya 14.

Ndipo ikafuata Jamhuri ya Pemba, timu pekee ya kisiwa hicho kufika fainali ya michuano hiyo ya Kombe la Mapinduzi, ikifanya hivyo mwaka 2012 kwa kukutana na Azam FC na kushindwa kuhimili vishindo vya Wana Lambalamba kwa kuchapwa mabao 3-1 na kuipa Azam taji la kwanza la michuano hiyo.

Mabao ya mchezo huo kwa Azam yalifungwa na John Bocco 41, Mrisho Ahmed akajifunga dakika ya 89 na Mrisho Ngassa akatupia la tatu katika dakika ya 90, wakati Ally Mmanga aliitanguliza Jamhuri kwa bao la dakika ya 16.

MIAKA 11 BAADAYE

Timu za Zanzibar ziliendelea kuwa wasindikizaji kwenye michuano hiyo kwa misimu 10 mfululizo tangu zilipocheza fainali kwa mara ya mwisho 2012, ndipo mwaka jana Mlandege ikafanya kweli kwa kutinga hatua hiyo.

Mlandege iliyoanza michuano iliyopita kwa sare ya 1-1 dhidi ya KVZ kabla ya kuifumua Simba kwenye mechi ya Kundi C, ilionyesha ilidhamiria kwani hata kwenye nusu fainali iliiduwaza Namungo kwa kutoka sare ya 1-1 kisha kwenda kuing'oa kwa mikwaju ya penalti 5-4 na kutinga fainali ambapo ilikutana na Singida iliyoifumua Azam kwa mabao 4-1.

Katika mechi hiyo, Mlandege ikiwa chini ya kocha Abdallah Mohammed 'Baresi' aliyepo Mashujaa kwa sasa, iliifumua Singida kwa mabao 2-1. Mabao ya timu hiyo yaliwekwa kimiani na Bashima Saite dakika ya saba na Abdulnassar Mohammed akaongeza la pili dakika ya 19. Bao la kufutia machozi la Singida lilifungwa na Fancy Kazadi aliyeibuka Mfungaji Bora alipotupia mpira wavuni katika dakika ya 51 na kufikisha mabao sita.

MSIMU HUU VIPI?

Mlandege hadi sasa bado haijawa na uhakika kama itavuka kwenda robo fainali ili kuweka hai matumaini ya kutetea taji, kwani tayari imeshashuka uwanjani mara mbili kwenye Kundi A na kuambulia suluhu mbele ya Azam kisha ikatoka sare ya 1-1 na Vital'O.

Kwa sasa imesaliwa na mechi moja itakayoikutanisha na Chipukizi, ili kuamua hatma ya kwenda robo fainali, imbapo huenda ikategemea pia kupita kwenye kapu la mshindwa bora (best looser) kutegemea na matokeo ya mechi za mwisho wakati Azam ikipepetana na Vital'O yenye alama mbili kama timu hiyo ya Zanzibar.

Azam yenyewe kwa sasa ndio inayoongoza kundi hilo ikiwa na pointi nne baada ya juzi usiku kushinda bao 1-0 mbele ya Chipukizi, huku Chipukizi ikiburuza mkia na alama moja, ambayo kama itashinda mechi ya mwisho inaweza kufikisha pointi nne pia na kusikilizia matokeo ya Azam na Vital'O kuona kama itaing'oa Mlandege au itafungasha virago kurudi Pemba.

Ukiondoa hali ya Kundi A kwa watetezi, lakini Kundi B, kuna vinara wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), JKU inayobeba dhamara ya kuipigania Zanzibar kundini humo ili kuhakikisha taji linasalia kwenye ardhi ya nyumbani.

Bahati mbaya ni kwamba JKU ilianza na mguu mbaya baada ya kufumuliwa mabao 4-1 na Singida na leo Jumatatu inarudi tena uwanjani kutesti zali mbele ya Simba kabla ya kumalizia mechi zao keshokutwa dhidi ya APR ya Rwanda, pambano litakalopigwa kuanzia saa 10:15 jioni kwenye Uwanja wa Amaan Complex.

KVZ NA JAMHURI

Kama itatokea Mlandege, Chipukizi na JKU zitachemsha kwenye makundi ziliyopo, basi kibarua kitakuwa mikononi mwa maafande wa KVZ na Jamhuri ya Pemba zilizopo Kundi C pamoja na Yanga na Jamus.

Timu hizo mbili za visiwani jana zilikuwa kibaruani kuvaana na wapinzani wao, huku KVZ ikiwa tayari ina pointi tatu ilizopata kwenye mchezo wa kwanza iliyocheza dhidi ya Jamhuri na kushinda mabao 2-0 yote yakifungwa na Akram Omar Muhina 'Haaland'.

Bila kujali matokeo ya jana, KVZ ikicheza na Jamus, huku Jamhuri ikiivaa Yanga, timu hizo zinakabiliwa na mechi za mwisho, Jamhuri dhidi ya Wasudan Kusini na KVZ kupepetana na Yanga ili kutoa washindi wawili wa kundi na nyingine moja ya best looser itakayochuana na wale wa kutoka makundi ya A na B.

Kwa namna ilivyo ni kwamba timu tano zilizopo Mapinduzi 2024 zote zina kazi kubwa ya kubeba heshima ya visiwa vya Zanzibar kwa kuhakikisha zinalibakisha taji hilo visiwani vinginevyo itakuwa noma kwa sherehe za Miaka 60 ya Mapinduzi kushuhudia taji likiondoka tena katika ardhi hiyo tukufu.

MAKOCHA, MASTAA

Kabla ya kuanza kwa michuano hiyo, makocha na wachezaji wa timu hizo tano za Zanzibar kwa nyakati tofauti walikaririwa kwamba wamepania msimu huu kufanya mambo na kubeba taji hilo ili kwenda sambamba na sherehe hizo za Miaka 60 ya Mapinduzi.

Kocha wa Chipukizi, Mzee Ali Abdallah alisema wamefanya maandalizi ya kuhakikisha taji linasalia Zanzibar na kwenda Pemba.

Nahodha wa timu hiyo, Abdul Mahafud Ali alisema hawana mzaha kwenye mashindano hayo watapiga mpira mwingi zaidi ya ule wa Ligi Kuu ili kutwaa ubingwa.

Alisema ingawa mashabiki hawana imani na timu za Pemba, msimu huu itakuwa tofauti na ilivyozoeleka, ila safari hii wajiandae kuona mambo, wakati Akram Omar wa KVZ, alisema licha ya kushiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza, lakini kasi aliyoanza nayo inampa matumaini ya timu hiyo kufanya kweli.

"Nashuruku kwa kuanza msimu wangu wa kwanza wa Mapinduzi kwa kufunga mabao mawili na kuiwezesha timu kuanza na ushindi, nadhani moto huu utaendelea hadi mwisho na In Shaa Allah tubebe ubingwa," alisema Akram maarufu kama Haaland.

Timu hizo za visiwani zimepata mzuka zaidi baada ya Kamati ya Mashindano ya Kombe la Mapinduzi kuongeza dau la zawadi kutoka Sh50 milioni zilizokuwa msimu uliopita na kufikia Sh100 milioni kwa bingwa huku mshindi wa pili akizoa Sh70 milioni badala ya 30 zilizotolewa msimu uliopita.

Pia kuwepo kwa zawadi ya Sh500,000 kwa Nyota wa Mchezo na Sh200,000 za Mchezaji Mwenye Nidhamu zimekoleza mzuka zaidi.

Hata hivyo, ngoja tuone hali itakuwaje? Timu za Zanzibar zinafukiza mashimo ya aibu za misimu kadhaa ya nyuma ama itaendelea pale ilipoishia Mlandege msimu uliopita. Tusubiri!

Chanzo: Mwanaspoti