Habari ndo hiyo. Tottenham Hotspur haitafanya haraka kutafuta mrithi wa kudumu wa Antonio Conte - licha ya kuwapo kwa makocha watatu mahiri kabisa ambao hawana kazi kwa sasa.
Antonio Conte aliachana na klabu ya Spurs usiku wa Jumapili iliyopita, lakini msaidizi wake Cristian Stellini amebaki kwenye kikosi hicho akipewa mikoba ya kuinoa timu hiyo kwa muda hadi mwisho wa msimu.
Mwenyekiti wa klabu hiyo, Daniel Levy atapitia kwa uangalizi mkubwa makocha wote wanaopewa nafasi ya kuchukua mikoba hiyo kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi kabla ya kumpata mmoja wa kumpa mikoba ya muda mrefu.
Mauricio Pochettino, Luis Enrique na Julian Nagelsmann - wanaopewa nafasi kubwa ya kupewa kibarua hicho, wote kwa sasa wapo huru, hawana kazi.
Spurs wanajipa muda zaidi kwa sababu wanaamini kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi huenda kukatokea nafasi ya makocha wengine makini zaidi wakapatikana.
Carlo Ancelotti amekuwa akielezwa juu ya uwezekano wa kuachana na Real Madrid, huku kukielezwa kwamba kuna klabu nyingine kama za Atletico Madrid, Paris Saint-Germain, AS Roma, Inter Milan na AC Milan - zinaweza kuingia sokoni kusaka makocha wapya kwenye dirisha hilo la majira ya kiangazi, ikiwa na maana kwamba huenda makocha kama Diego Simeone wakawa wanapatikana sokoni.
Pochettino, Enrique na Nagelsmann watafikiriwa zaidi na Spurs kama hakutakuwa na mabadiliko yeyote. Lakini, kwa kitendo cha Spurs kusubiri hadi mwisho wa msimu hilo litawafanya kuingia kwenye vita kali dhidi ya wengine wanaowataka makocha hao.
Bayern Munich tayari imeshamchukua Thomas Tuchel baada ya kumfuta kazi Nagelsmann.
Makocha wengine wanaodaiwa huenda wakawa sokoni mwisho wa msimu ni Marco Silva, Ange Postecoglou, Ruben Amorim na Roberto De Zerbi waliopo kwenye ajira zao kwa sasa.
Conte, 53, baada ya kuondoka Spurs - jina lake litakuwa kwenye mchakato mkubwa wa kupewa kazi huko Italia. Hadhi yake inaweza kutibuka kwa upande wa England hasa kwa kile kilichotokea Spurs, lakini huko kwao Italia jina lake bado lipo juu sana, mahali ambako mara ya mwisho alibeba ubingwa wa Serie A alipokuwa na Inter mwaka 2021.
Wengi walitarajia Conte ataondoka na benchi lake lote, lakini ni ndugu yake tu, Gianluca Conte, ambaye ni mchambuzi wa kiufundi ndiye waliyetoka wote wakiachana na Spurs. Lakini, kocha wa makipa, Marco Savorani, mtaalamu wa mipira iliyokufa Gianni Vio na makocha wa viungo Stefano Bruno na Costantino Coratti wamebaki na kumsaidia kocha wa muda Stellini katika mechi 10 za mwisho walizobakiza kwenye Ligi Kuu England. Mikataba yao itamalizika mwisho wa msimu.
Kocha wa kikosi cha kwanza, Ryan Mason atakuwa msaidizi wa Stellini na wawili hao wote wamekuwa wakikubalika sana kwenye kikosi hicho kutokana na kushiriki mara nyingi mazoezi na wachezaji.
Conte alifunguliwa mlango wa kutokea baada ya kuwabwatukia wachezaji na mabosi wa timu hiyo, akisema wachezaji ni wabinafsi baada ya kupoteza uongozi wao wa mabao 3-1 na kupata sare ya 3-3 dhidi ya Southampton Jumamosi iliyopita.
Mashabiki wa Spurs wamemshukuru Conte kwa upambanaji wake, lakini wamemtaka mwenyekiti Levy kuteua kocha ambaye atafundisha kwa staili na kufuata utamaduni wa klabu hiyo.