Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi amefichua kuwa anataka kuona timu yake inashinda mechi tatu za ligi ambazo ni sawa na dakika 270 kabla ya kumalizika kwa mwaka huu ili kujiweka katika wakati mzuri wa kuwania ubingwa wa msimu huu.
Yanga ambayo inaongoza ligi kwa pointi 20 wakifuatiwa na Simba ina mechi tatu za Ligi Kuu Bara kabla ya kumalizika kwa mwaka huu.
Yanga kesho Jumapili itacheza mchezo wake wa kwanza dhidi ya Prisons kabla Desemba 26, mwaka huu kucheza dhidi ya Biashara United na Desemba 31, mwaka huu itamaliza na Dodoma Jiji.
Akizungumza Nabi amesema kuwa wamerejea kwenye ligi baada ya mchezo wa Kombe la Shirikisho lakini malengo yake ni kuona wanashinda mechi tatu zilizobakia kwenye ligi kabla ya kuisha kwa mwaka huu ili kupunguza presha na pengo la matokeo ya mechi walizotoka sare kwa kuwa wana malengo ya ubingwa.
“Tumerejea kwenye ligi ambayo ndiyo ina malengo yetu makuu msimu huu kwa sababu tunapigania ubingwa ambao kila timu inapambana kuona inafanya kitu cha tofauti maana tuna mechi tatu kabla ya kuisha kwa mwaka ambazo tunaziangalia kwa utofauti mkubwa.
“Matarajio ni kuweza kushinda mechi zote tatu kabla ya kumalizika kwa mwaka kitu ambacho tayari kila mmoja ndani ya timu anakijua nini ambacho tunakilenga kwenye mechi hizo tukianza na Prisons kisha Biashara halafu Dodoma, naamini tutakuwa sehemu salama,” alisema Nabi.