Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nabi na heshima yake Yanga

Mashabiki Wa Yanga Mkapa Nabi na heshima yake Yanga

Thu, 16 Mar 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi ni kama ametega bomu ambalo litawachukua muda mrefu makocha wa timu nyingine na hata watakaoinoa timu hiyo baadaye kuja kulitegua kwa namna alivyoandika rekodi za kibabe hadi sasa.

Nabi ambaye ilibaki kidogo afungashiwe virago Jangwani, pamoja na kuvunja rekodi tamu zilizokuwa zimedumu klabuni na katika Ligi Kuu Bara ikiwa ni pamoja na kuvunja rekodi ya kocha ambaye pia alifanikiwa kuipatia mafanikio makubwa Yanga, Hans Van Pluijm ambaye sasa anainoa Singida Big Stars.

Nabi ametengeneza rekodi yake ndani ya Yanga ambayo inaonyesha anaweza kuwatesa wenzake kwa muda mrefu, kwani kocha huyo amedhihirisha jina la utani la Profesa hakulipata kwa kubahatisha.

Kocha huyo ameiongoza Yanga kuvunja rekodi ya Azam FC ya kucheza mechi 38 mfululizo za Ligi Kuu bila kupoteza huku akijiwekea rekodi yake ya kucheza mechi 48 bila kufungwa na kufanikiwa kutwaa taji la ligi baada ya miaka minne.

Lakini tofauti na Azam ambayo wakati inaweka rekodi ya kutopoteza mechi 38 ilikuwa chini ya makocha wawili tofauti, Nabi amefikia rekodi hiyo akiiongoza Yanga akiwa pekee na mara ya mwisho kupoteza ilikuwa ni dhidi ya Ihefu FC Novemba 29 baada ya Azam kuifunga Yanga Aprili 25, 2021 bao 1-0.

Wakati Azam inacheza mechi 38 bila kupoteza, ilinolewa na Stewart Hall ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Joseph Omog. Hall aliiongoza Azam kucheza michezo 21 bila kupoteza kabla ya kutimuliwa Novemba, 2013 nafasi yake ilichukuliwa na Omog ambaye chini yake, Azam ilicheza mechi 13 za Ligi Kuu bila kupoteza hadi Oktoba 25, 2014 ilipofungwa bao 1-0 nyumbani na JKT Ruvu ambayo sasa ni JKT Tanzania.

Katika mechi 49, ambazo Nabi ameiongoza Yanga Ligi Kuu bila kupoteza, timu hiyo imeibuka na ushindi michezo 36 na sare 12.

USHINDI MICHEZO 36

Katika michezo 49, ambayo Yanga imecheza bila ya kufungwa imeshinda mechi 36 tu iliyoshinda kuanzia huku 12 iliyobaki ikiisha kwa sare.

Japo Azam ilidumu na rekodi yake kwa miaka minane, lakini rekodi ya Yanga imeifanya ijipe ugumu yenyewe na hata kwa timu nyingine, kuweza kuirudia tena siku za baadaye kwa idadi hiyo ya mechi na ushindani mkali ulioongezeka katika ligi nchini.

Kwa ujumla Azam katika mechi zake 38, ilishinda 26 na kutoka sare 12, ikifunga mabao 72 na kuruhusu nyavu zao kuguswa mara 21 na kuvuna jumla ya pointi 90.

MECHI 11 MFULULIZO

Baada ya Ihefu FC kuikandamiza Yanga na kuvunja rekodi ya kutokufungwa mechi 48 ikiwafunga mabao 2-1 Nabi amejitengenezea ufalme mwingine kwa kushinda mechi 11 mfululizo akikusanya pointi 33 ikifunga mabao 21.

Rekodi hiyo ilianza dhidi ya Tanzania Prisons, Yanga ikishinda bao 1-0, ikashinda 2-0 dhidi ya Namungo, 3-0 dhidi ya Polisi Tanzania, ikaifunga Coastal Union 3-0, ikashinda 3-2 dhidi ya Azam FC, iliifunga Mtibwa Sugar 1-0, ikalipa kwa Ihefu kwa kuifunga 1-0, iliifunga Ruvu Shooting 1-0, 2-0 dhidi ya Namungo, KMC ilikubali kichapo cha bao 1-0 na juzi imeifunga Geita Gold mabao 3-1 imebakiza mechi sita kumaliza msimu.

NABI KAFUNGWA MBILI TU

Nabi alitua nchini Aprili 20 kumalizana na Yanga tayari kwaajili ya kurithi mikoba ya Cedric Kaze aliyetimuliwa kabla ya kurudishwa tena kuwa msaidizi wake.

Kocha hiyo tangu ametua nchini na kuanza majukumu ya kuinoa Yanga amefungwa mechi mbili tu hadi sasa akiwa tayari ameipa taji moja na yupo kwenye nafasi nzuri ya kutetea taji hilo msimu huu.

Nabi ameiongoza Yanga kupoteza dhidi ya Azam FC 1-0 na Ihefu FC iliwalaza kwa mabao 2-1.

DHIDI YA SIMBA, AZAM

Kwenye kila safari ya mafanikio huwezi kukosa vikwazo ndivyo Yanga ilivyokutana na michezo migumu wa ‘Dabi ya Karikoo’ kutoka kwa Simba na ule wa Azam. Yanga ilikutana na Simba mara nne ikishinda moja (1-0) Julai 3, 2021, kisha mechi mbili zikaisha kwa suluhu Desemba 11, 2021 na Aprili 30, 2022 na sare ya 1-1 Oktoba 23, 2022.

Kwa upande wa Azam ambayo ndiyo iliyoifunga Yanga zimekutana mara nne ikifungwa miwili (2-0) Oktoba 30, 2021, (2-1) Aprili 6, 2022 na sare moja ya 2-2 Septemba 6, 2022 na ushindi Desemba 25, 2022 (2-3).

POINTI SABA CAF

Achana na rekodi ya kumfunga Mwarabu ugenini na kupata nafasi ya kutinga hatua ya makundi ikiifunga Club Africain kutokeaTunisia bao 1-0, pia Yanga ilifanikiwa kuvunja uteja kwa TP Mazembe kwa kuifunga mabao 3-1 nyumbani unaambiwa baada ya muda mrefu Nabi avunja rekodi.

Katika awamu tatu tofauti zilizopita Yanga ikishiriki makundi ya mashindano ya klabu Afrika, idadi kubwa ya pointi ilizowahi ikikusanya ni nne na kujikuta wakiburuza mkia kwenye makundi iliyopangwa.

Chini ya Nabi timu hiyo imeweka rekodi nyingine ya kupata ushindi katika mechi mbili za makundi kwani hapo awali, ilipata ushindi mara moja tu ikiwa ni sare moja na kufikisha idadi ya pointi saba.

REKODI ZA PLUIJM

Msimu wa 2016, Hans Van aliiwezesha Yanga kutwaa Kombe la FA baada ya kushinda mechi zote saba toka mechi za mtoano, robo fainali, nusu fainali na fainali dhidi ya Azam FC.

Hii ni jumla ya mechi 29 kati ya mechi 37 katika Ligi Kuu na na FA, Pluijm aliiwezesha Yanga kushinda kwa msimu wa 2015-16.

Hatua ya awali ya klabu bingwa barani Afrika Pluijm aliiwezsha Yanga kushinda mechi tatu. Alishinda dhidi ya Cercle de Joachim nyumbani na ugenini ikiwa ni jumla ya mechi mbili pia akishinda mechi moja dhidi ya APR na kutoka sare mechi ya marudiano jijini Dar.

Hatua ya pili klabu bingwa alikwenda sare mara moja dhidi ya Al Ahly jijini Dar ( 1-1 ) na kufungwa 2-1 jijini Alexandria Misri. Hii ni wastani wa kushinda mechi tatu klabu bingwa, sare mbili na kufungwa mechi moja.

Kombe la Shirikisho Hans Van Pluim aliiongoza Yanga ambayo ilipoteza mechi nne za makundi ikifanikiwa kushinda mechi moja na kutoka sare moja.

Msimu wa 2016/17, Ligi Kuu Tanzania Bara mechi ya Ngao ya Jamii alipoteza kwa matuta dhidi ya Azam FC.

Chanzo: Mwanaspoti