Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nabi kiboko yao

Nabi Pic Xxx Nabi kiboko yao

Mon, 9 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Hivi unaposoma habari hii, kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi ametimiza jumla ya siku 624 tangu alipoanza kuinoa timu hiyo akiwa ameiongoza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara moja, Ngao ya Jamii mara mbili, Kombe la Shirikisho la Azam mara moja lakini pia kuiongoza kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.

Kana kwamba haitoshi, takwimu zinaonyesha katika mashindano ya ndani ambayo Nabi ameiongoza Yanga, timu hiyo imepoteza mechi tatu tu ambazo mbili ni za Ligi Kuu na moja ni ya Kombe la Shirikisho la Azam na zilizobakia ni ama imeibuka na ushindi au kutoka sare.

Achana na dondoo hizo za hapo juu, Nabi ameibuka na jambo lingine la kibabe ambalo hakuna kocha yeyote wa timu ya Ligi Kuu ya NBC ambaye ameweza kulifanya katika kipindi cha siku 624 ambazo Mtunisia huyo ameiongoza Yanga.

Ubabe huo wa Nabi ni ule wa kuwa kocha pekee ambaye hajaonja ladha ya kutimuliwa tangu alipotua hapa nchini kwa mara ya kwanza.

Tangu Nabi alipoanza kuinoa timu hiyo, Yanga ndio timu pekee ambayo hadi sasa haijabadilisha kocha mkuu huku nyingine 15 zikiwa zimeshabadilisha makocha kuanzia wawili na kuendelea.

Nabi ameshuhudia makocha wenzake wa timu nyingine wakibadilishwa na kuletwa wengine ambao baadhi humuacha huku yeye akiendelea kutamba katika viunga vya Jangwani.

Katika kipindi cha siku 624 ambazo Nabi amedumu Yanga, Simba imenolewa na makocha watano tofauti ambao ni Didier Gomez, Hitimana Thiery, Pablo Franco, Juma Mgunda na sasa Robertinho Olivieira wakati Azam imenolewa na makocha wanne tofauti ambao ni George Lwandamina, Abdihamid Moalin, Denis Lavagne na Dani Cadena.

Mtibwa Sugar yenyewe imekuwa chini ya makocha wanne tofauti ambao ni Zubery Katwila, Salum Mayanga, Hitimana Thiery na Joseph Omog, Singida Big Stars imenolewa na Ramadhan Nsanzurwimo na Hans Pluijm, wakati Namungo FC imekuwa chini ya Hemed Morocco, Honor Janza na sasa Denis Kitambi.

Kwa upande wa Kagera Sugar imekuwa chini ya Francis Baraza na Mecky Maxime, Geita Gold imenolewa na Etienne Ndayiragije na Felix Minziro, KMC yenyewe imeongozwa na John Simkoko na Hitimana Thiery wakati Mbeya City imeongozwa na Mathias Lule na Abdallah Mubiru.

Maafande wa Tanzania Prisons wamenolewa na Salum Mayanga, Patrick Odhiambo na Mohamed Adolph 'Rishard, Dodoma Jiji imeongozwa na Mbwana Makata, Masoud Djuma na sasa, Melis Medo wakati huo Ihefu ikiwa chini ya Katwila na Juma Mwambusi kwa nyakati tofauti.

Wana Mangushi, Coastal Union wao wamenolewa na makocha wanne tofauti ambao ni Juma Mgunda, Melis Medo, Yusuph Chipo na Joseph Lazaro, Ruvu Shooting imeongozwa na Makata pamoja na Charles Boniface Mkwasa huku Maafande wa Polisi Tanzania wakiongozwa kwa nyakati tofauti na makocha Joslin Bipfubusa.

Akizungumzia kudumu kwake ndani ya Yanga, kocha Nabi alisema ni kutokana na imani kubwa ambayo klabu imeweka kwake.

"Nawashukuru viongozi, benchi la ufundi, mashabiki na wachezaji kwa ushirikiano mkubwa ambao wamekuwa wakinipatia. Haya yasingetokea kama tusingekuwa tunashirikiana. Naamini tutafanikiwa zaidi kama tukiendelea kuwa pamoja," alisema Nabi.

Chanzo: Mwanaspoti