Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nabi hasumbuki na uvumi wa Fei toto kuondoka Yanga

Nabi Na Fei Toto Nabi hasumbuki na uvumi wa Fei toto kuondoka Yanga

Wed, 7 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati uvumi ukiendelea kusambaa kuwa kiungo wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’ anatingisha kibiriti cha kutaka kutimka katika timu hiyo, kocha wake Nasreddine Nabi ameibuka na kusema sio viongozi wa klabu yao wala wadhamini wanaweza kuruhusu kitu hicho kutokea.

Akizungumza baada ya Fei Toto kuipa pointi tatu timu hiyo akifunga bao safi dhidi ya Tanzania Prisons, Nabi alisema mchezaji huyo hawezi kuondoka klabuni hapo.

Nabi ambaye yuko nje akitumikia adhabu ya kusimamishwa mechi tatu na Bodi ya Ligi aliyoanza dhidi ya Prisons, alisema kama kuna mahitaji yanayohitajika kuongezeka kwa Fei Toto uongozi wa Yanga hauwezi kushindwa kufanya hivyo kwa kuwa wanajua thamani ya kiungo huyo uwanjani.

“Tukiwa kama timu tunathamini kila nguvu ya kila mchezaji wa timu yetu. Hii ni familia na Feisal ni mmoja wa wanafamilia. Sote tunafahamu juu ya ubora wake kwa sasa ni vigumu kujaribu hata kufikiri kwamba ataondoka hapa kirahisi hivyo,” alisema Nabi.

“Napenda sana kufanya kazi na wachezaji wazawa wa taifa hili kwa kuwa sasa nipo hapa. Tukiwa wakweli unapozungumza wachezaji bora wa taifa hili huwezi kuacha kumtaja wa kwanza Feisal. Yuko katika kiwango bora.

“Sidhani kama kuna kiongozi wa Yanga au hata wadhamini wetu GSM wanaweza kujadili hili la kumuacha aende timu nyingine. Hapa sioni hilo na zaidi bado ana mkataba mrefu. Kama kuna kitu juu ya maslahi yake hilo linaweza kumalizwa kirahisi na uongozi ambao una malengo makubwa.”

Kauli hiyo ya Nabi inakuja kufuatia uvumi kuwa Azam FC inamnyemelea kiungo huyo ingawa kupitia Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Abdulkarim Amin ‘Popat’ imekanusha taarifa hizo ikidai hazina ukweli wowote.

Nabi aliwataka wachezaji wengine wa timu hiyo kuiga mwendelezo wa kiwango bora kinachoonyeshwa na Fei uwanjani akisema hatua hiyo itakuza ushindani katika kikosi chao.

“Unakumbuka kiwango cha Feisal msimu uliopita? Angalia pia msimu huu.. angalia jana (juzi), alitoka majeruhi lakini ari yake katika kuipigania timu ni kubwa. Tunahitaji kuwa na watu wenye mwendelezo kama huo wa kutunza viwango vyao,” alisema kocha huyo aliyeiongoza yanga kushinda mechi 49 mfululizo Ligi Kuu.

Msimu huu Fei Toto amefanikiwa kufunga mabao matano akitoa asisti mbili katika michezo 12 aliyocheza sawa na dakika 802.

Chanzo: Mwanaspoti