Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nabi fundi sana, apewe maua yake

NABI MAYELE NA AZIZ Nabi fundi sana apewe maua yake

Thu, 15 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Namba hazidanganyi. Namba hazijawahi kuongopa, hata iwe vipi! Na hivi ndivyo kazi kubwa ya Kocha Nasreddine Nabi ilivyo. Ufanisi wake, upo wazi hata kwa mtu asiyejua soka.

Alipotua nchini Aprili mwaka 2021. Alikaribishwa na kipigo cha bao 1-0 kutoka kwenye mechi ngumu dhidi ya Azam. Bao la dakika ya 86 kutoka kwa Prince Dube aliyefumua shuti la mbali, lilitosha kumzindua akili na kumfahamisha amekuja kwenye nchi yenye ushindani mkubwa kisoka.

Akili akaziweka sawa na kuiongoza Yanga baada ya hapo alicheza mfululizo mechi 49 bila kupoteza, zilizojumuisha michezo saba za kumalizia msimu wa 2020-2021, kisha akaunganisha tena mapambano 30 za msimu wa 2021-2022.

Baada ya kuiongoza Yanga kubeba ubingwa wa Ligi Kuu bila kupoteza mchezo wowote kwa msimu huo, alianza tena kuwasha moto kwenye michezo 12 mfululizo ya msimu wa 2022-2023 kabla ya ye ule wa 13 kukumbana na kipigo cha 2-1 kutoka kwa Ihefu na kumtibulia rekodi ya kufikisha mechi 50.

Baada ya kipigo hicho cha fedheha alichokumbana nacho Novemba 29, 2022, Nabi alilipanga jeshi lake na kucheza tena michezo 12 bila kupoteza hadi alipocharazwa na Simba Aprili 16, mwaka huu na kumalizia mechi tano za mwisho za kufungia msimu bila kupoteza na kutetea taji kwa msimu wa pili.

Rekodi zinaonyesha kwenye mechi 67 za Ligi Kuu, Nabi aliiongoza Yanga kushinda ugenini jumla ya michezo 25 kati ya 34 iliyocheza chini yake, ikitoka sare saba na kupoteza mechi mbili tu, huku ikivuna mabao 51 na yenyewe kufungwa 18 na kukusanya pointi 82. Kwanini asiitwe Profesa!

Kwa mechi za nyumbani sasa, Nabi nako amefanya kufuru kwa kuchza 33, akishinda 27 na kutoka sare sita na kutopoteza hata mara moja, akivuna jumla ya mabao 70 na kufungwa 12 tu akizikusanya pointi 87.

SIO HUKO TU

Kama unadhani Nabi aliotea tu kwenye Ligi Kuu kwa misimu hiyo miwili na kidogo, utakuwa umekosea kwani hata kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho (ASFC) nako ana balaa lake.

Kocha huyo Mbelgiji mwenye asili ya Tunisia, aliiongoza Yanga kwenye michezo 15, huku akipoteza mechi moja tu, ambayo ni ile fainali ya msimu wa 2020-2021 alipoikuta timu katikati na kwenda kulala 1-0 mbele ya Simba katoika pambano lililopigwa, Lake Tanganyika mjini Kigoma.

Kabla ya kupoteza fainali hiyo kwa bao la kiungo mkabaji kutoka Uganda aliyekuwa Msimbazi wakati huo Taddeo Lwanga, Nabi aliiongoza Simba kwenye michezo mitatu ukiwamo wa 16 Bora dhidi ya Tanzania Prisons na kushinda 1-0, kisha kuinyuka Mwadui kwa 2-0 kwenye robo fainali na ilipotinga nusu fainali ikainyoa tena Biashara United kwa bao 1-0 ndipo ikaenda kufa Kwa Mnyama.

Msimu uliopita wa michuano hiyo akiwa ndio injinia wa kila kitu, Nabi alishinda mechi zote sita ikiwamo ya fainali dhidi ya Coastal Union aliowanyoa kwa penalti 4-1 baada ya dakika 120 kuisha kwa sare ya 3-3. Kabla ya fainali alianza kwa kuichapa Ihefu kwa mabao 4-0 hatua ya 64 Bora, kisha kuifunga Mbao kwa bao 1-0 kwenye 32 Bora na kwenye 16 Bora ikaichapa Biashara United kwa 2-1.

Hatua ya robo fainali iliitambia Geita Gold kwa penalti 7-6 baada ya dakika 90 kuisha kwa sare ya 1-1 na kutinga nusu fainali iliyowakutanisha na watani wao, na kuwachapa bao 1-0 ikiwavua taji na kwenda fainali iliyopigwa Sheikh Amri Abeid na kuwanyoosha Wagosi wa Kaya ak.a Wanamangushi.

Kwa msimu huu ilianza kampeni ya kutetea taji kwa kugawa dozi ya 8-0 kwa Kurugenzi Kigoma, kisha kuinyoa Rhino Rangers kwa 7-0 na kwenye 16 Bora ikaitambia Tanzania Prisons kwa mabao 4-1 na ilipotinga robo fainali ikaifanyizia Geita Gold kwa 1-0 na nusu fainali ikaing'oa Singida Big Stars pia kwa bao 1-0, kisha juzi kati tu pale Mkwakwani, Tanga ikailaza Azam kwa bao 1-0 na kubeba taji.

KIMATAIFA

Kwenye anga la kimataifa Nabi, alianza vibaya msimu wake wa kwanza akiwa na Yanga kwa kupoteza nje ndani kwenye mechi za raundi ya awali dhidi ya Rivers United ya Nigeria kwa bao 1-0 na kuzua maneno kibao dhidi yake kabla ya kujipanga kwa msimu uliopita ambapo amefanyia sifa.

Nabi alianza mechi za Ligi ya Mabingwa kwa kuifumua Zalan FC ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 9-0, ikishinda 5-0 na 4-0 na kufuzu raundi ya kwanza ambapo iling'olewa na Al Hilal ya Sudan kwa kutoka sare nyumbani 1-1 kisha kulala 1-0 ugenini na kuangukia kwenye play-off ya Kombe la Shirikisho ikipangwa na Club Africain na kutoka suluhu nyumbani na kushinda ugenini 1-0.

Katika hatua ya makundi Nabi aliongoza vijana wake kushinda mechi nne na kutoka sare moja, huku ikipoteza mchezo mmoja tu dhidi ya US Monastir ya Tunisia na kutinga robo fainali ambapo katika hatua hiyo ilishinda 2-0 ugenini na kutoka suluhu nyumbani na kwenye nusu ilishinda 2-0 na 2-1 dhidi ya Marumo Gallants ya Afrika Kusini na kutinga fainali kwa mara ya kwanza kwenye historia ya Yanga na timu za Tanzania kwenye michuano hiyo tangu ilipobadilishwa kuanzia mwaka 2004.

Katika mechi ya kwanza ililala nyumbani 2-1 na kushinda ugenini 1-0 dhidi ya USM Alger ya Algeria ambao walibeba taji hilo kwa sheria ya bao la ugenini japo matokeo ya jumla ilikuwa ni sare ya 2-2.

Kama hujui kwenye mechi za kimataifa za CAF, Nabi ameiongoza Yanga kwenye michezo 20 na kushinda 11, kutoka sare nne na kupoteza mara tano, ikivuna jumla ya mabao 28 na kufungwa 11 tu na na kama ni pointi kutokana na matokeo hayo basi imevuna jumla ya alama 37 kati ya 60 ilizohitajiwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live