Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nabi azidi kupandisha presha Yanga, asakwa Uarabuni

Nabi Nasreddine Prof Nasreddine Nabi

Mon, 6 Mar 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kikosi cha Yanga kinaendelea na maandalizi ya mchezo ujao wa Kundi D la michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Real Bamako ya Mali, huku kocha wa timu hiyo, Nasreddine Nabi akichomoa tetesi za kuifundisha Taifa Stars.

Kocha huyo amewashusha presha mashabiki wa Yanga, lakini ghafla limeibuka jambo jingine ambalo limewafanya mabosi wa klabu hiyo kuanza kukuna vichwa baada ya klabu kubwa mbili barani Afrika kumsaka ili akazifundishe.

TP Mazembe ya DR Congo imeweka nguvu kutaka kumrudisha kocha huyo nchini humo, lakini sasa ikitaka aendee Lubumbashi baada ya awali kufanya kazi Kinshasa akiwa na DC Motema Pembe.

Tajiri wa klabu hiyo iliyopo kundi moja na Yanga katika Kombe la Shirikisho na iliyokubali kipigio cha mbao 3-1 jijini Dar es Salaam, Moise Katumbi anadaiwa kumtaka kocha huyo baada ya kufanya usajili mkubwa ambao anaona bado haujazaa matunda kimataifa.

Katumbi anaona Mazembe haijapata kocha sahihi, baada ya kocha na nahodha wa zamani wa klabu hiyo, Pamphil Mihayo kuwa na kasi ndogo na kumfanya awe na presha kila timu inaposhuka uwanjani.

Mazembe inaona haiwezi kupasua ikiwa na Mihayo na Mwanaspoti linafahamu kuwa tajiri huyo amempigia simu Nabi akimtaka kufikiria kufanya kazi na klabu yake akimuahidi malipo ya kufuru yatakayomfanya kuwa kocha anayelipa fedha nyingi.

Katumbi hataki Mazembe ififie hasa wakati huu akipiga hesabu za kuwania urais wa nchi hiyo ambapo anatamtaka Nabi kwenda kurudisha jina lake kabla ya mbio hizo za ndoto zake za kuwa Rais hazijachanganya.

Achana na Katumbi, Waarabu wa Tunisia, nchi anayotoka kocha huyo wa Yanga, nao wametajwa kumfukizia Nabi ili arudi nchini humo.

Klabu ya CS Sfaxien kupitia mabosi wake nayo haikauki kumtwangia simu ya kocha huyo ikimshawishi kurejea nyumbani huku ikimuahidi fedha ndefu kama atakubaliana na mkataba wao.

Sfaxien inaona haina kocha sahihi wa kuirudishia nguvu kupambana na Esperance ya hapohapo kwao ambao msimu huu iko kwenye moto mkali chini ya Kocha Nabil Maaloulikishinda mechi zote tatu za Ligi ya Mabingwa hatua ya makundi.

Hiyo inakuwa ni klabu ya pili ndani ya wiki tatu kutoka Tunisia kumhitaji Nabi, kwani awali ilitangulia Etoile du Sahel ambayo baada ya kumsaka kocha huyo na kushindwa, juzi ilimpa ajira kocha mkongwe wa nchini humo Faouzi Benzarti.

Taarifa za Nabi kusakwa na klabu hizo zenye fedha za kumwaga zimefanya mabosi wa Yanga kuanza kukuna vichwa licha ya kutambia mkataba walioingia nao hivi karibuni kuwapa jeuri.

Mwanaspoti lilizungumza na kocha huyo juu ya dili hizo, alisema kwa sasa yuko bize kuona Yanga inatinga robo fainali ya michuano ya CAF. Yanga ina kibarua cha kurudiana na Real Bamako ya Mali, Jumatano Uwanja wa Benjamin Mkapa baada ya awali kutoka nao sare ya 1-1 jijini Bamako, kisha itaialika US Monastir ya Tunisia Machi 19.

Mbali na kibarua hicho, Nabi anakabiliwa na mtihani wa kuhakikisha anashinda mechi nne mfululizo za Ligi Kuu Bara ikiwamo na Simba Aprili 9 ili kutetea taji kwa msimu wa pili mfululizo kwani kwa sasa inaongoza msimamo ikiwa na pointi 62.

Chanzo: Mwanaspoti