Yanga tayari ipo nchini ikitokea Nigeria ilikoshinda ugenini kwa mabao 2-0 dhidi ya wenyeji wao Rivers United, lakini kocha wao akawaambia wasahau walishinda mchezo wa kwanza na sasa kazi inaanza upya.
Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi ameliambia Mwanaspoti amefanya kikao maalumu na wachezaji wake kabla timu yao haijaanza safari ya kuondoka nchini Nigeria na ujumbe wake mkubwa ni wafute matokeo ya ushindi wa kwanza.
Nabi alisema licha ya timu yake kushinda ugenini lakini bado wapinzani wao wanahitaji kuheshimiwa kutokana na ubora wao ambao wanaweza kuja kupindua matokeo endapo watawadharau.
"Nimewaambia wachezaji wangu furaha ya ushindi iliishia pale geti la uwanja tulioutumia kucheza ile mechi, sitaki kuona mchezaji yeyote akiendelea kufurahia ule ushindi, ile mechi imekwisha, ni sawa na tumecheza dakika 45 za kipindi kimoja na hapa tunakuja kucheza dakika 45 za kumalizia mchezo," alisema Nabi.
"Huu ujumbe wangu naomba pia uwafikie mashabiki wetu, wajue kazi haijamalizika, kama tukifanya makosa ya kujisahau tunaweza kuja kupata mshtuko mbaya, tunatakiwa kushinda haraka katika mchezo ujao Jumapili.
"Watu wanatakiwa kujua kuna wachezaji ambao wapinzani wetu hawakuwatumia katika mchezo wa kwanza tuliambiwa wanaumwa nani anajua kama wakija kucheza hapa wataibadilisha timu yao nafikiri tahadhari ni muhimu sana."
Aidha Nabi aliongeza kikosi chake kinachoingia kambini haraka leo jioni kitakuwa na maandalizi makubwa kuelekea mchezo huo wa marudiano utakaopigwa Jumapili Aprili 30, kuhakikisha wanashinda mechi hiyo.
"Hii sio timu rahisi ndio maana mnaona tulikuwa na mabadiliko ya mifumo mara mbili katika mchezo wa kwanza, hata hii mechi ya pili tunaweza kuwa na mabadiliko makubwa yatakayotufanya tutafute ushindi bila kusababisha hatari ya ushindi wetu wa kwanza.
"Tunatakiwa kuwa na nidhamu kubwa uwanjani kama ambavyo tulifanya ugenini, kama kuna kitu tunatakiwa kuwa nacho makini ni kuwaruhusu wapinzani wetu kupata bao hapa."
Yanga inatakiwa kupatab ushindi wowote, sare au kuruhusu kufungwa bao moja ili iweze kufuzu nusu fainali kwa mara ya kwanza kwenye historia ya timu hiyo.