Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nabi awatega wachezaji Yanga, Ndondo marufuku

Kaze Nabi Makocha wa Yanga, Kaze na Nabi

Tue, 5 Jul 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi amesema baada ya kutimiza lengo la kutwaa ubingwa wa mashindano yote matatu makubwa nchini, anawapa mapumziko ya wiki mbili nyota wake, kisha kuja kuanza upya kazi wakianzia pale walipoishia ili kukamilisha malengo ya msimu mpya.

Yanga ilirejea juzi jioni kutoka Arusha ilipotwaa ubingwa wa ASFC kwa kuifunga Coastal Union kwa penalti 4-1 baada ya kumaliza dakika 120 kwa sare ya mabao 3-3 na Kocha Nabi alisema kwa vile hakuna muda kabla ya maandalizi ya msimu mpya anatoa mapumziko mafupi.

Alisema atawapa mapumziko yasiyozidi wiki mbili wachezaji wake ili kila mmoja kwenda nyumbani kwake kukaa na familia yake kabla ya kuwaita kwa ajili ya kwenda kambini.

“Wachezaji wangu wamefanya kazi kubwa na nzuri msimu huu kuchukua mataji yote matatu si kazi ndogo, wanahitaji kupumzika pamoja na familia zao ikiwemo kupongezana ila haitakuwa zaidi ya wiki mbili,” alisema Nabi na kuongeza;

“Wanastahili kupata muda wa kutosha zaidi ya huo lakini mashindano ya CAF, yapo karibu kuanza tunahitaji kupata muda wa kutosha kufanya maandalizi ili kukwepa historia mbaya ya kuondolewa hatua ya awali kama ilivyokuwa msimu uliopita.

“Sitaki kuona wachezaji wanajihusisha na mpira huko walipo mapumzikoni kwani nataka wakirejea kila mmoja awe na hamu ya kufanya mazoezi kwani tutakuwa nayo magumu katika siku za mwanzo kwenye (pre-season).

Nabi alisema anataka wachezaji waendeleze pale walipoishia ili kuendelea kuwapa raha mashabiki aliowashukuru kwa kuwaunga mkono mwanzo mwisho na kufanikisha kung’ara kwa kikiosi hicho kubeba mataji matatu (treble).

Alisema kutokana na kuwa na mipango mipya kwa msimu ujao, wachezaji wote waliosajiliwa na Yanga msimu huu wanatakiwa kuwepo Dar.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz