Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nabi awataka Simba Ngao ya Jamii

Sure Boy Na Kocha Nabi Nabi alishinda Ngao ya Jamii dhidi ya Simba SC msimu uliopita

Wed, 10 Aug 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Yanga inaangalia zaidi mechi ijayo ya Ngao ya Jamii dhidi ya watani wao, Simba ambapo kocha Nasredine Nabi amesema amepata namna gani ya kuingia uwanjani siku hiyo, Agosti 13, mwaka huu Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.

Hivi karibuni Yanga ikiwa inahitimisha tamasha la Wiki ya Mwananchi, timu hiyo ilicheza na mabingwa wa Ligi Kuu Uganda, Vipers ambao walishinda mabao 2-0, hivyo matokeo hayo Nabi amesema anayatumia kama njia ya kutafuta tiba kuelekea mechi ya watani.

Nabi alisema Yanga itacheza mechi ngumu dhidi ya Simba na kwa maana hiyo makosa yaliyotokea mchezo uliopita anayafanyia kazi mazoezini ili kubadilika.

Alisema kuna vitu vya kiufundi wachezaji walivikosa na vingine walishindwa kuvifanya haraka, jambo ambalo lilikuwa faida kwa Vipers kuwafunga.

“Muda wa kufanya maandalizi ulikuwa mfupi kwani siku chache zilizopita tulikuwa tumetoka kufanya mazoezi mengi magumu. Kwa maana hiyo miili ya wachezaji ilikuwa haijafunguka na walikosa uharaka katika uamuzi. Mabao tuliyofungwa yalitokana na hilo,” alisema.

“Hata msimu uliopita tulikutana na changamoto kama hii ila muda mfupi tulifanya maandalizi mengi ya usahihi ndani yake na tuliifunga Simba mechi ya Ngao ya Jamii, naamini itakuwa hivyo hata msimu huu.

“Nafahamu ukubwa na ugumu wa mechi, ila ushindi kwetu una maana kubwa ya kufanya vizuri msimu ujao kwani morali itakuwa kubwa kwa wachezaji kama ambavyo tulianza msimu uliopita.

“Kama ambavyo Simba wanatufuatilia ili kuhakikisha wanafanya maandalizi kulingana nasi, tulivyo hata upande wetu ni vivyo hivyo lengo kubwa ni ushindi upatikane na kutetea taji hili.”

Katika hatua nyingine Nabi alisema anafahamu Simba ya msimu ujao itakuwa tofauti kulingana na usajili ilioufanya na maboresho ya benchi la ufundi, hivyo itakuwa mechi yenye ushindani mkubwa.

“Benchi kuna makocha wazuri kama Mtunisia Karim Sbai namfahamu siku nyingi anaweza kutimiza majukumu yake ila wamejipanga na wapo tayari kupambana nao.

“Tunaendelea na maandalizi ya kutosha kiwango ambacho kilionekana kwetu kitakuwa tofauti na kile ambacho tulionyesha mechi iliyopita. Tutabadilika ili kuhakikisha tunapata ushindi,” alisema Nabi.

“Hakuna mechi ya Dabi katika nchi yoyote ile inakuwa nyepesi na hilo ndio litatokea hata kwenye mechi huo.” Msimu uliopita Simba ilifungwa bao 1-0 na Yanga katika mechi ya ufunguzi wa msimu ya Ngao ya Jamii - bao la Yanga likifungwa na Fiston Mayele.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live