Aliyekuwa Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi amesema atarudi rasmi kuwaaga mashabiki wa timu hiyo katika kilele cha Wiki ya Wananchi, lakini akazima presha ya kwamba atasepa na wachezaji wa timu hiyo kwenda kwenye timu anayotajwa kuhusishwa nayo ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
Nabi aliyeifundisha Yanga tangu Aprili 21, 2021 hadi Juni 14, 2023 amekataa kuongeza mkataba mpya na Yanga baada ya ule wa mwaka mmoja kumalizika na anatajwa kutakiwa na Kaizer Chiefs na Wanayanga wana presha huenda akaondoka na baadhi ya mastaa ili kwenda kuendeleza moto Sauzi.
Kipa Diarra Djigui na Fiston Mayele ni kati ya wachezaji wanaotajwa huenda wakasepa na Nabi kwenda Sauzi kutokana na kiwango kikubwa walichoonyesha kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika wakiifikisha timu hiyo kwenye fainali na kupoteza mbele ya USM Alger ya Algeria.
Hata hivyo, akizungumza na Mwanaspoti juzi, Nabi alisema hana mpango wa kuibomoa timu hiyo kwa kuondoka na wachezaji wake bora kwenye kikosi cha timu hiyo.
Nabi alisema hataki kugeuka adui wa Yanga kwa kuwaondoa mastaa wa timu yake waliompa mataji saba ndani ya miaka miwili na kwamba kuondoka kwao labda kuweka na hesabu zao binafsi.
"Hapana kuondoka na wachezaji wa Yanga hilo halipo kwenye akili yangu, kwanza sijajua hata wapi nakwenda sasa siwezi kuwashawishi wachezaji kuondoka hapa," alisema Nabi na kuongeza;
"Siwezi kugeuka mtu mbaya kwa klabu ninayoipenda, nawaheshimu sana mashabiki wa Yanga unajua naondoka lakini moyo wangu unaniambia baki Yanga isipokuwa akili tangu ndio inanisisitiza hebu ondoka kwasasa hapo ulipo.
"Kuchukua wachezaji wa Yanga ni kuwaumiza watu hawa nilioishia nao vizuri, siwezi kusema wachezaji hawawezi kuondoka, lakini kama wataondoka iwe kwa hesabu zao wenyewe na sio mimi."
Hadi sasa kuna taarifa kwamba wachezaji watatu wameomba kuondoka Yanga, akiwamo Joyce Lomalisa, Djuma Shaban, Yannick Bangala, huku Mayele naye ikielezwa anajiandaa kutimka baada ya kupata dili nono nje ya nchi ikitajwa ni Sauzi na nchi moja ya Kiarabu, japo mabosi wa Yanga wanapambana kuhakikisha mambo yakaenda sawa kwa lengo la kutoyumbisha mafanikio waliyonayo.