Yanga iko kazini ikijiandaa na mechi mbili, moja ni leo ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo kabla ya kusafiri kwenda Tunisia kuifuata US Monastir katika mchezo wa makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika na juzi kocha wa timu hiyo, Nasreddine Nabi alikuwa akiwapa mbinu mpya safu ya ushambuliaji inayoongozwa na Fiston Mayele na ile ya mabeki iliyo chini ya Yannick Bangala.
Kwanza utambue kuwa, dozi ya mazoezi ya timu hiyo juzi ilipunguzwa kidogo kutoka ile ya mara mbili kwa siku yaani asubuhi na jioni na kupugwa asubuhi tu. Ratiba hiyo ilianzia Jumatatu wiki hii na kuishia juzi Jumatano, huku kazi ya nguvu ikifanyika kwa kila kipindi kimoja wakitumia dakika 150.
Lakini kazi ambayo ilikuwa inafanyia kuanzia juzi ni kusuka safu yao ya ushambuliaji kwa kocha Nabi na msaidizi wake, Cedric Kaze wamekuwa wakimwaga mbinu mbalimbali za kuhakikisha washambuliaji wao pamoja na mawinga wanakuwa na makali ya kufunga na kutengenezeana nafasi.
Kwa ubora wa mawinga Jesus Moloko,Tuisila Kisinda, Dickson Ambundo na mastraika Fiston Mayele aliye moto kwa sasa sambamba na Kennedy Musonda basi beki ya Namungo ijipange.
Kwenye mazoezi hayo washambuliaji hao kila mmoja alifunga mara tatu huku makocha wakionyesha kutaka utulivu zaidi kwa kutoridhika na mabao hayo.
Ukiacha kuisuka safu hiyo pia kulikuwa na kazi nyingine kwenye ratiba hiyo kusuka safu yao ya ulinzi ili isiruhusu mabao, huku Kaze alikuwa akifanya kazi kubwa na Nabi akiwa na muda wa kuongeza kitu pale anapoona kuna kitu hakiendi sawa.
Mabeki hao wamekuwa wakijaribiwa kwa kutengenezewa mashambulizi makali huku makocha wao wakiwapa mbinu washambuliaji wao katika kuwasoma makosa wanayoyataka kuyarekebisha kwa mabeki wao.
Katika mazoezi hayo yaliyofanyika kambini Avic Kigamboni, beki mpya Mamadou Doumbia naye alikuwa na kipengele chake akiwa anajaribiwa kucheza na mabeki watatu kwa nyakati tofauti.
Doumbia ambaye bado hajacheza hata dakika moja ya mechi ya ligi, zaidi ya dakika 45 za mechi ya Kombe la Shirikisho (ASFC), alikuwa akijaribiwa kucheza na mabeki Yannick Bangala, Dickson Job na Bakari Mwamnyeto katika kuangalia nani anaelewana naye vyema
Hata hivyo, beki huyo bado hajaweza kuchanganya sawasawa ukilinganisha na wenzake hao ambao tayari wameshaanza kuelewana kwa muda mrefu.
Yanga itarudi Kwa Mkapa leo kuikaribisha Namungo ambao ilikubali kichapo nyumbani kwao Lindi cha mabao 2-0 kwenye mchezo wa kwanza, kisha akili yao itaanza kufikiria mechi ya kwanza wa makundi ya Shirikisho Afrika dhidi ya US Monastir utakaopigwa Februari 12, jijini Tunis.