Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nabi awaka Yanga SC, Makambo OUT

Fei Na Nabi.jpeg Nabi awaka Yanga SC, Makambo OUT

Wed, 28 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Yanga juzi ilifikisha alama 47 kileleni mwa Ligi Kuu baada ya kuichapa Azam mabao 3-2, kwenye mechi ya raundi ya 18 lakini kocha wake mkuu Nassredine Nabi amewawakia mastaa wa timu hiyo akitaka wajitume zaidi na waongeze umakini ili kuhakikisha wanatetea ubingwa wao walioutwaa msimu uliopita kwa mara ya 28.

Mbali na kuwawakia pia taarifa inasema kuwa juzi Nabi alikuwa na kikao na wachezaji wake na benchi la ufundi akitaka ishu ya Fei Toto waiweke pembeni kwanza na kuwaza kuisaidia timu yao kupata ushindi.

Mabao makali ya Fiston Mayele, Stephane Aziz Ki na Farid Musa, yaliyoipa Yanga ushindi kwenye mchezo huo hayajamfanya Nabi kushindwa kuona upungufu wa chama lake na kuamua kuwachana wachezaji wake ili mechi zijazo wawe bora zaidi.

Nabi amechimba mkwara huo baada ya Azam kuonekana kuwa bora zaidi yao kiuchezaji hususani eneo la kiungo na kuifanya Yanga iruhusu mabao mawili na yote yakifungwa na Abdul Seleman ‘Sopu’ aliyewafunga ‘hat trick’ msimu uliopita kwenye fainali ya Kombe la ASFC, akiwa na Coastal Union.

Akizungumza Nabi amekiri kuona udhaifu wa wachezaji wake hususani eneo la kiungo wa ukabaji na mabeki pale wanapokutana na timu inayoshambulia zaidi kama Azam na kuahidi kulifanyia kazi haraka iwezekanavyo suala hilo huku akiwataka wachezaji waongeze morali ya upambanaji bila kudharau mechi.

“Azam imetupa changamoto sana hususani eneo la kiungo na la juu, walikuwa bora na kutengeneza nafasi nyingi ambazo kama wangezitumia kwa usahihi huenda wangeshinda mechi ya leo (juzi),” alisema Nabi na kuongeza;

“Sio jambo zuri kwetu kwani tuna mechi nyingi mbele, wachezaji wanapaswa kuongeza hali ya upambanaji na umakini katika maeneo yao, naamini wanaweza kuwa bora zaidi pia hawapaswi kukubali kuwa dhaifu na kupitika kirahisi kama ilivyokuwa leo (juzi), tunatakiwa kuongeza umakini zaidi.

“Naenda kuongea nao na kuwaeleza hili na naamini watalichukua na zaidi tutalifanyia kazi ili kuimarika na kuhakikisha makosa kama yale hayajirudii.”

Mbali na hilo taarifa inasema kuwa uongozi pamoja na benchi la ufundi, kabla ya mechi ya juzi walikaa na wachezaji wao wakizungumza nao kuwa wanatakiwa kurudisha mawazo kwenye mechi na kuachana na suala la Fei Toto ambaye ametangaza kuvunja mkataba wake na Yanga.

MAKAMBO OUT

Habari za ndani zinasema mabosi wa Yanga watavunja mkataba wa Heritier Makambo na nafasi yake ikitarajiwa kujazwa na Yacouba Sogne aliyerejea kutoka kuwa majeruhi, huku Lazarous Kambole akisubiri kwanza.

Mwanaspoti linafahamu Namungo ilikuwa ni moja ya klabu zilizomhitaji Makambo, lakini mshahara wake wa Dola 5,000 uliwashinda.

Chanzo: Mwanaspoti