Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nabi awaingiza chaka Al Hilal

Yanga Mapro Nabi awaingiza chaka Al Hilal

Wed, 28 Sep 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kocha Mkuu wa Yanga, Mtunisia, Nasreddine Nabi, amewaambia wapinzani wake Al Hilal ya Sudan, wasifikirie kwamba atapanga kikosi na kutumia mfumo, mbinu kama alizotumia dhidi ya Zalan FC, badala yake, anakuja kivingine.

Kauli hiyo ameitoa wakati Yanga ikiwa kambini ikijiandaa na mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal utakaopigwa Oktoba 8, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar.

Yanga imefanikiwa kufuzu hatua ya kwanza ya michuano hiyo baada ya kuiondosha Zalan ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 9-0, huku mshambuliaji wa timu hiyo, Mkongomani, Fiston Mayele akipiga hat trick mbili.

Nabi alisema Wanayanga wasihofie kuelekea mchezo dhidi ya Al Hilal ya Sudan na wala wasiogopeshwe na ubora wa wapinzani wao hao.

Nabi alisema katika michezo miwili dhidi ya Al Hilal, ataingia uwanjani tofauti na alivyocheza dhidi ya Zalan ili kuhakikisha anapata ushindi na kufuzu hatua ya makundi kwenye michuano hiyo inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Aliongeza kuwa, mashabiki wa timu hiyo, watarajie kuona mabadiliko ya kikosi chake cha kwanza na aina ya soka watakalocheza baada ya kufanya maboresho katika baadhi ya sehemu ikiwemo safu ya ushambuliaji ambayo ilishindwa kutumia nafasi nyingi za kufunga licha ya kupata ushindi mnono dhidi ya Zalan.

“Sina hofu yoyote kuelekea mchezo dhidi ya Al Hilal, sio kwamba nawadharau wapinzani wetu, hapana, ni timu nzuri iliyofanya usajili mkubwa huku ikiongowa na kocha wa viwango vya kufundisha soka Afrika ambaye ni Ibenge (Florent).

“Ninaamini wapinzani wetu wametuona katika michezo miwili tuliyocheza ya hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zalan ambayo tuliwafunga mabao 9-0.

“Hivyo wameona udhaifu wetu, hivyo niwaambie kama kocha nimepanga kuingia uwajani kucheza dhidi ya Al Hilal kitofauti kabisa kwa kubadili kikosi, mbinu na aina ya mfumo nitakaoutumia.

“Hiyo ni baada ya ongezeko la kiungo wetu mpya Kisinda (Tuisila) katika safu ya ushambuliaji, ninaamini uwepo wake kutaimarisha kikosi changu na kupata matokeo mazuri na kufuzu hatua inayofuatia,” alisema Nabi.

Kabla ya kucheza na Yanga, Al Hilal inatarajiwa kwenda DR Congo kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya TP Mazembe ikiwa ni sehemu ya kujiweka sawa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live