Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nabi atoboa siri anayopitia Mwamnyeto Yanga

Mwamnyeto Bakari Bb Mfungaji wa moja ya magoli mchezo wa jana

Tue, 4 Oct 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Mashabiki wa Yanga bado hawamwelewi nahodha wa timu hiyo, Bakari Mwamnyeto msimu huu, baadhi yao wakimshambulia kwenye mitandao ya kijamii kwamba ameishiwa, lakini kocha mkuu wa timu hiyo, Nasreddine Nabi amevunja ukimya na kumkingia kifua akieleza kilichompunguza kasi.

Mbali na kueleza sababu za kiufundi zilizomkwamisha Mwamnyeto, lakini kocha huyo aliamua kuwaonya mashabiki wa timu hiyo kutomchukulia poa beki huyo wa kati mwenye mwili jumba.

Akizungumza Nabi alisema Mwamnyeto bado ni mchezaji muhimu na anastahili heshima kubwa licha ya wakati mgumu anaoupitia sasa akipambana kurudisha kiwango chake bora.

Nabi alisema beki huyo amekuwa akitumika mfululizo ndani ya kikosi hicho kwa miaka miwili huku pia akiwa katika kikosi cha kwanza cha timu ya taifa na kuchangia kumchosha kiakili na kimwili.

“Nimeona watu wanamuandama sana Mwamnyeto (Bakari), bahati mbaya wako hadi mashabiki wetu, kwangu hii sio sawa, huyu ni nahodha wetu hapa ambaye ametupigania kwa miaka miwili mfululizo bila kuchoka,” alisema Nabi na kuongeza;

“Wakati nafika hapa nimemkuta Mwamnyeto anacheza kikosi cha kwanza akiwa katika ubora mkubwa, wakati huohuo alikuwa mchezaji muhimu katika ukuta wa timu ya taifa kila mchezo wa timu hiyo alicheza bila kupumzika, huyu ni binadamu anachoka, tulipaswa kuwa naye pamoja kila wakati na sio kumchoka.

“Ni kweli amepunguza kasi yake kutokana na kuchoka, ndio maana nasi tunampumzisha kwa kuwa timu ina watu wa kucheza nafasi yake, akiimarika tutaendelea kumwamini ni mmoja kati ya wachezaji bora hapa tulionao.”

Aidha Nabi alieleza mbali na changamoto za uwanjani beki huyo alikuwa akiuguliwa na baba yake mzazi hatua ambayo ilimpa msongo mkubwa wa mawazo.

“Sikupaswa kulieleza hili lakini watu wafahamu kuna wakati mchezaji anaweza kukutana na mambo magumu hata nje ya uwanja, alikuwa akiuguliwa na mzazi wake, tumekuwa tukijitahidi sana kuwa naye karibu na hata kumsaidia na tunaona anaimarika taratibu, masahabiki wetu wanatakiwa kuwa pamoja naye wakati huu.

“Kila mchezaji anaweza kukumbwa na mchoko na wakati mgumu kama Mwamnyeto ila ni afya tukiwapa nguvu na muda wa kurudisha na nguvu zaidi badala ya kuwaponda.”

Katika hatua nyingine winga Tusila Kisinda leo anaanza rasmi kazi Yanga katika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Ruvu Shooting.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz