Kocha Mkuu wa Yanga, Nasredinne Nabi amesema amefurahishwa na mafanikio aliyoyapata ndani ya klabu hiyo huku akiwatuliza mashabiki juu ya uwepo wake ndani ya timu hiyo.
Hayo ameyasema leo Jumatatu baada ya kumalizika kwa mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam ambapo wametetea ubingwa huo kwa kuifunga Azam bao 1-0 kwenye Uwanja wa Kwakwani jijini hapa.
Hivi karibuni kumekuwepo na tetesi za kumalizika mkataba wa kocha huyo hivyo mashabiki wa klabu hiyo wakiwa njiapanda kuhusu kubaki ama kuondoka.
Hofu kubwa ni kwamba Nabi anadaiwa kuwa na ofa nyingi na ni rahisi kuondoka kwani hatabanwa na mkataba wake.
"Tulijiandaa kushinda na kutetea kombe hili ingawa wachezaji wangu wamechoka sana kutokana na kucheza mechi mfululizo ingawa tuliambizana kupambana kushinda.
"Lakini kuhusu mimi naomba hili litajulikana hapo baadaye kwasasa tunasherehekea ubingwa tulioupata, Wanayanga tunapaswa kusherekea haya na mengine yatafuata baadaye, kwani hakuna kitu kinachoweza kujificha," amesema Nabi