Kocha mkuu wa Yanga, Nassredine Nabi amesema wana kila sababu ya kuchukua pointi tatu katika mchezo wao wa kesho dhidi ya Polisi Tanzania.
Polisi Tanzania wataikaribisha Yanga kesho katika mchezo utakaopigwa katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha saa 10:00 jioni.
Akizungumza na Waandishu wa habari, Nabi alisema anatambua ugumu wa wapinzani wao lakini wamejiandaa kuondoka na pointi tatu.
“Polisi Tanzania sio timu ya kawaida wapo vizuri na wanasumbua timu nyingi, tumejiandaa kuchukua pointi tatu katika mchezo huu,” amesema Nabi.
Nabi amesema kwenye mchezo huo kunaweza kuwa na mabadiliko kidogo kutokwna na kiungo wake Feisal Salum kupata matatizo kidogo ya kiafya.
“Kutakuwa na mabadiliko kidogo kutokana na afya ya Feisal, nitaangalia uwezekano wa Mukoko(Tonombe) kucheza na hata Chico (Ushindi) nitaangalia dakika za kumpa katika mchezo huu,” amesema Nabi na kuongeza;
“Kwenye mechi ya kirafiki nimetumia kuwapa nafasi wachezaji wasiocheza Ligi na wale wapya ili wote wapata utimamu wa mwili.”
Kwa upande wa Polisi, kocha msaidizi wa timu hiyo George Mketo amesema licha ya kubadilishwa kwa uwanja hakuondoi kwao kupambana na Yanga.
Mketo amesema walijiandaa vizuri kuhakikisha wanapata matokeo mazuri mbele ya Yanga na kuwapa furaha mashabiki wao.
“Tunacheza na timu inayoongoza Ligi, tumejiandaa vizuri na tuna wachezaji wenye uzoefu wa kutosha hivyo tutatoka na pointi tatu,” amesema Mketo.