Kocha Mkuu wa AS. FAR Rabat ya Morocco, Nasreddine Nabi ameitaka klabu hiyo kuhakikisha inainasa saini ya mlinzi wa Simba SC na timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Henock Inonga.
Nabi ambaye aliwahi kuwa kocha wa Young Africans, anahitaji saini ya Inonga kuimarisha kikosi chake kwa michuano mbalimbali msimu huu.
Dirisha dogo la usajili nchini Morocco lilifunguliwa Januari 3, mwaka huu na linatarajiwa kufungwa keshokutwa Jumatano (Januari 31).
Taarifa zinadai kuwa, Nabi amependekeza kusajiliwa beki huyo ambaye yupo katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) inayoendelea Ivory Coast ambapo timu yake ya DR Congo jana usiku ilifanikiwa kutinga Hatua ya Robo Fainali kwa kuifunga Misri katika mchezo wa 16 Bora.
Inonga ambaye amebakisha mwaka mmoja katika mkataba wake na Simba SC, ameripotiwa kuwa na thamani ya sh. bilioni 1.2.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani kutoka AS FAR Rabat, Nabi raia wa Tunisia, ameuambia uongozi huo kuwa, anahitaji saini ya Inonga kuimarisha kikosi chake.
“Nabi amewaambia mabosi wa timu yake Kuhakikisha wanaipata saini ya beki huyo (Inonga) ikiwa ni maboresho ya kikosi chake, ingawa wanatambua hali halisi ya thamani ya mchezaji na bado ana mkataba na Simba SC unaotarajiwa kufikia ukingoni mwakani,” chanzo hiko kimesema.
Hata hivyo Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema hawezi kuongea jambo lolote kwa kuwa bado klabu haijapokea ofa yoyote mezani inayomhusisha Inonga.
“Sisi kwa sasa hatuna jambo lolote la kusema kama ni kweli au vipi kwa sababu uongozi bado hauna ofa yoyote inayomhusisha Inonga na klabu yoyote zaidi tunaendelea na maandalizi ya ligi,” amesema Ahmed Ally.
Ameongeza kuwa, nyota huyo mkataba wake unamalizika mwakani na ikitokea ofa imefika mezani kwao, suala la kumuuza au kuendelea naye litakuwa kati ya benchi la ufundi linaloongozwa na Abdelhak Benchikha, mchezaji mwenyewe na uongozi.