Kocha wa zamani wa Yanga, Nasreddine Nabi amebakiza mechi kumi kutwaa taji la Ligi Kuu Morocco 'Botola Pro 1' akiongoza kwa pointi 46 akiwa na mchezo mmoja mkononi.
Nabi ambaye anainoa FAR Rabat ya nchi hiyo ameiongoza timu yake kwenye mechi 20 ikifuatwa nyuma na Raja Casablanca ambayo imecheza mechi 21 ikikusanya pointi 45.
FAR ya kocha huyo wa zamani wa Yanga imefikisha pointi 46 baada ya kushinda mechi jana iliyoitandika Union Touarga Sportif 'UTS' mabao 3-0.
Nabi kwenye mechi 20 alizoiongoza timu yake ameshinda mechi 14, sare nne na kupoteza mbili hivyo endapo atashinda mechi zote zilizobaki na mpinzani wake Raja Casablanca akashinda zote atamuacha nyuma kwa pointi tano.
Kocha huyo ambaye aliifikisha Yanga kwenye hatua ya fainali Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita, licha ya kuongoza ameshindwa kutamba na timu hiyo kimataifa kwani alijikuta akiondolewa mapema katika hatua ya mtoano.
Nabi aliondoka nchini akiwa tayari ameipa Yanga mataji mawili ya Ligi Kuu Bara mfululizo na taji moja la Ngao ya Jamii na Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).
Pia aliiongoza Yanga kucheza michezo 48 ya Ligi Kuu Bara bila kupoteza ambapo kati ya hiyo alishinda 36 na kutoka sare 12 wakati Yanga ilipoweka rekodi ya kibabe ya kucheza mechi 49 bila ya kupoteza katika ligi nalba ya kuachana na kikosi hicho msimu uliopita na nafasi yake kuchukuliwa na Muagentina, Miguel Gamondi Juni 24, mwaka jana.