Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nabi anawatesa tu huko Morocco

Kocha Nabi Msz Kocha Nasreddine Nabi.

Wed, 13 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Aliyekuwa kocha wa zamani wa Yanga akiacha rekodi nzuri, Nasreddine Nabi ameendeleza makali yake nchini Morocco, baada ya kushinda mechi sita mfululizo na kuwaacha wababe Raja Cassablanca kwa pointi nne katika mbio za kutetea taji.

Nabi kwa sasa anainoa FAR Rabat ya Morocco inayoongoza msimamo kwa pointi 55 baada ya kucheza mechi 23 sawa na Raja Cassablanca (51) ikiwaacha nyuma vigogo wawili wa nchini humo Wydad yenye pointi (33) nafasi ya tano na RS Berkane (33) nafasi ya sita baada ya kucheza mechi 21.

Kocha huyo amejihakikishia nafasi ya kuongoza msimamo na kufikisha pointi hizo baada ya jana usiku akiwa ugenini kuizamisha Youssoufia Berrechid kwa mabao 2-0.

Kwa mujibu wa msimamo wa Ligi Kuu nchini Morocco, FAR Rabat imeshinda mechi 17, sare nne na vipigo wiwili kwenye mechi 23 ilizocheza hadi sasa huku ikifunga mabao 52 na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara 16.

Nabi tangu ametua kwenye timu hiyo ameiongoza kwenye mechi zote 23, huku katika zile sita alizoshinda mfululizo amefunga jumla ya mabao 15 na kuruhusu mabao mawili tu. Alianza kushinda dhidi ya Renaissance Zemamra ugenini (1-0), Mouloudia Oujda nyumbani (5-0), Union Tourga nyumbani (3-0), IR Tanger ugenini (1-2) RCB Berkane ugenini (1-2) na jana (juzi) 2-0 dhidi ya Youssoufia Berrechid.

Akizungumza na Mwanaspoti, Nabi alisema ana furaha kufundisha timu ambayo ameikuta ina kikosi imara na sasa inampa matokeo mazuri ikiwa na malengo ya kutetea taji lake msimu huu.

"Sio rahisi kupata matokeo hasa ukicheza ligi ambayo ina timu kubwa na zenye mafanikio mazuri, nafikiri kikosi imara kilichopo ndio siri ya mafanikio haya ambayo yananipa nguvu ya kuendelea kupambana kuandika rekodi," alisema.

Kocha huyo ambaye aliifikisha Yanga hatua ya fainali Kombe la Shirikisho Afrika, ameshindwa kutamba na FAR Rabat kimataifa baada ya kuondolewa mapema katika hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Afrika akishinda mechi mbili kati ya nne.

REKODI ZA NABI YANGA Nabi aliondoka nchini akiwa tayari ameipa Yanga mataji sita, mawili ya Ligi Kuu Bara mfululizo, mawili ya Ngao ya Jamii na mawili ya Kombe la Shirikisho.

Ukiondoa rekodi hizo pia aliipeleka Yanga hatua ya fainali kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ikishindwa kutwaa taji kutokana na kanuni ya mabao mabao mengi ya ugenini.

Nabi aliiongoza Yanga kuweka rekodi ya taifa ya kucheza mechi 49 za Ligi Kuu Bara bila ya kupoteza akishinda mechi 37 na kutoka sare mechi 12 akiipiku kwa mbali rekodi ya mechi 38 za bila ya kichapo iliyoshikiliwa na Azam FC kwa miaka minne.

Azam FC katika rekodi yake ya kucheza mechi 38 bila ya kupoteza, ilishinda 26 na kutoka sare 12, ikifunga mabao 72 na kuruhusu nyavu zake kuguswa mara 21 na kuvuna jumla ya pointi 90.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live