Kama hufahamu ni kwamba kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi ni rafiki mkubwa wa kocha wa Taifa Stars, Adel Amrouche lakini Kuna kitu kinatengenezwa pale Yanga kitamfaa.
Kwa mchezo wa pili sasa Nabi ameanza kwa mafanikio na ukuta mzima wa wachezaji wazawa pekee kasoro kipa kisha wakafanya kazi ya kibabe.
Kuanzia mchezo wa marudiano kati ya wenyeji Yanga dhidi ya Rivers United ya Nigeria, Nabi alianza na beki wa kulia Dickson Job, shavu la kushoto akapewa Kibwana Shomari huku vitasa wa kati wakiwa nahodha Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Hamad 'Bacca'.
Ukuta huo kwenye mchezo huo walipiga kazi ya nguvu na kushindwa kuruhusu bao lolote na kuifanya Yanga kutoka salama wakifuzu hatua ya Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Kama haitoshi Nabi akaurudia ukuta huo huo juzi wakicheza na Singida Big Stars ambapo ukuta huo ukaitoa Yanga na uongozi wa mabao 2-0 dakika 45 za kwanza kabla ya kipindi cha pili kupanguliwa kidogo.
Nabi kipindi cha pili alimpumzisha Job nafasi yake ikachukuliwa na Mkongomani Djuma Shaban akirejea kwenye nafasi yake huku wengine wakiumaliza mchezo huo. Kiwango cha mabeki hao kinaweza kuwa habari njema kwa Amrouche ambaye tayari alishaanza kuwatumia mabeki hao watatu kati ya wanne.
Akizungumzia hatua hiyo, Nabi alisema mabadiliko hayo yametokana na hesabu za kimbinu pia kutoa muda wa wengine kupumzika kwa kuwafanyia mzunguko.
"Tunapompa nafasi mchezaji kuanza hakuna maana yule asiyeanza ana matatizo hapana inawezekana tunaona timu tunayocheza nayo inahitaji mabeki ambao watakuwa na ubora mkubwa wa kuzuia kuliko kushambulia sana.
"Kikosi changu kina baraka za kuwa na mabeki wenye ubora wa kushambulia vizuri lakini pia wapo wengine wao wanaanza na kuzuia kisha kushambulia baadaye.
"Kwasasa pia lazima mjue kuna wachezaji wamecheza sana msimu huu lazima tuwapatie muda wa kupumzika vizuri wakati huo wengine nao wanacheza, tunakaribia mwisho wa msimu wapo ambao watakuwa wametumika kuliko wengine kwahiyo huu mzunguko unatuimarishia timu yetu, kitu nafurahia wanaoanza na hata wanaoingia bado ubora wao ni mkubwa."