Kocha Mkuu wa Yanga, Mtunisia Nasreddine Nabi amemsihi kiungo fundi wa Klabu hiyo, Feisal Salum 'Fei Toto' kufanya maamuzi kwa utashi wake na si kutokana na kundi la watu wanaomzunguka.
Nabi amesema hayo jana Jumapili, Februari 19, 2023 wakati akizungumza na wanahabari mara baada ya mchezo wa yanga dhidi ya TP Mazembe ya Congo DR ambapo Yanga aliibuka na ushindi wa bao 3-1.
Feisal aliandika barua mwishoni mwa mwaka jana 2022 akiomba kuondoka Yanga jambo ambalo lilimuingiza kwenye mgogoro na uongozi wa timu yake na kusababisha kufika katika mamlaka za TFF kwa ajili ya usuluhishi ambapo TFF iliamua kuwa Fei ni mchezaji halali ya Yanga.
Hata hivyo, mwishoni mwa wiki iliyopita, zilitoka taarifa kuwa tayari Yanga wameshafikia makubaliano ya kumuongezea mshahara Mzanzibar huyo na kwamba muda wowote atarejea Jangwani.
"Feisal ni mchezaji mkubwa, ambaye pia alikuwa na mchango mkubwa kwenye timu. Morrison pia ni mchezaji mkubwa, ambaye naye ana mchango miubwa kwenye Yanga. Lakini sisi tuna timu, hawa waliocheza leo wametetea vyema nembo ya Yanga kwa leo, wamejitolea na tumepata matokeo mazuri.
"Tutafurahi Feisal akirudi ama akifanya maamuzi yake yeye kama Feisal kwa utashi wake na si kwa sababu ya kundi la watu wachache wanaomzunguka. Atakapochukua maamuzi yake yeye kama Feisal haina shida," amesema Kocha Nabi.