Kama dili la aliyekuwa kocha wa Yanga Nasreddine Nabi na Kaizer Chiefs halitatimia, inaonekana kuwa timu hiyo itamchukua kocha wa Mamelodi Sundowns, Manqoba Mngqithi.
Mangoba alikuwa akiitumikia Mamelodi kuanzia mwaka 2022, akiwa ndiye kocha wao mzoefu na amekuwa akihusishwa na timu kadhaa mara kwa mara ikiwemo Kaizer.
Baadhi ya magazeti ya Afrika Kusini likiwemo The South African, leo yamekuwa yakiripoti kuwa mazungumzo kati ya Kaizer na kocha huyo yanaendelea baada ya timu hiyo hadi sasa kushindwa kukubaliana na Nabi.
Hata hivyo, wakala wake Mike Makaab amesema bado mteja wake ni muajiriwa wa Mamelodi na anafurahi kubaki hapo kwa mwaka mwingine mmoja.
Nabi ambaye aliipa Yanga makombe matatu msimu uliopita na kuifikisha hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, amekuwa akipewa nafasi kubwa ya kuchukua nafasi ya Arthur Zwane wa Kaizer, ingawa inaonekana kuwa timu hiyo inashindwa kufikia muafaka kutokana na Nabi kutaka kwenda na wasaidizi wake.
Kama watashindwana jumla inaonekana kuwa Mngqithi atapewa jukumu hilo kwa kuwa anakwenda mwenyewe.