Kocha Mkuu wa Young Africans Nasreddine Nabi amekiri kuwa katika wakati mgumu, kuelekea mchezo wa mzunguuko wa nne wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam FC, utakaochezwa Jumamosi (Oktoba 30) Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Young Africans inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu kwa kufikisha alama 9, itakuwa mwenyeji wa mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini kote, kutokana na ubora wa vikosi vya pande zote mbili.
Kocha Nabi amesema kikubwa anachohitaji ni alama tatu za mchezo huo, na lazima wachezaji wake wavuje jasho katika kuzipambania ndani ya uwanja, jambo ambalo anaona linawezekana kutokana na ubora wa kikosi chake.
Amesema ana imani na wachezaji wake kwa sababu hadi sasa hawajapoteza mchezo wowote, hivyo watahakikisha wanaingia uwanjani kwa tahadhari kubwa kwa sababu unapozitaja timu nne bora kwenye Ligi ya Tanzania Bara, lazima utaigusa Azam FC.
“Hawajaanza vizuri, lakini hawa ni washindani kwenye mbio za ubingwa, mechi itakuwa ngumu kwetu, nimewaona walivyocheza na wao pia wametuona, nadhani itakuwa mechi ya mbinu na kiufundi zaidi ingawa nina matumaini ya kushinda,” amesema Nabi.
Amesema wanaendelea na mazoezi kujiandaa na mchezo huo na wakipambana kusahihisha baadhi ya mapungufu ambayo wameyaona kwenye michezo iliyopita.
Mara ya mwisho timu hizo zilipokutana Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam msimu uliopita 2020/21, Young Africans ililala kwa bao 1-0 lililofungwa na Mshambuliaji wa Azam FC Prince Dube dakika ya 85.