Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nabi aifungia kazi Al Hilal

NABI IBENGE Nabi aifungia kazi Al Hilal

Tue, 11 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, ameamua kuifungia kazi Al Hilal ya Sudan baada ya kuipigisha timu yake mazoezi mara mbili kwa siku, huku akieleza kuwa anatarajia kufanya kweli ugenini.

Awali, Yanga kabla ya kucheza mechi ya kwanza dhidi ya Al Hilal walikuwa wakifanya mazoezi mara moja kwa siku na baada ya kupoteza mechi hiyo, Nabi amewafungia kazi wachezaji wake kwa kuwapa program maalum kuelekea mchezo huo wa marudiano utakaopigwa Jumapili wiki hii jijini Khartoum, Sudan.

Kikosi cha Yanga kinatarajia kuondoka keshokutwa, Alhamisi kuelekea Khartoum, Sudan kwa ajili ya mchezo huo ambao wanahitaji kupata ushindi wowote ama sare ya kuanzia mabao mawili ili kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Akizungumzia hilo jana, Nabi alisema amerejea uwanjani kwa ajili ya kufanyia kazi mapungufu yao kwa kuelekea kupambania matokeo chanya katika mechi hiyo ya marudiano.

Alisema wanaendelea na maandalizi kwa kufanya mazoezi mara mbili kwa siku ambapo asubuhi wanafanya saa mbili na nusu na jioni.

"Tumeona madhaifu yetu katika mechi yetu ya hapa nyumbani, sasa tumeyabeba hayo na kufanyia kazi kuhakikisha tunakisuka kikosi imara kumalizia dakika 90 zilizobakia," alisema Nabi.

Katika hatua nyingine Kiungo wa Yanga, Feisal Salum amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa Septemba wa Ligi Kuu Bara huku Kocha wa Namungo FC, Honor Janza akichaguliwa kuwa kocha bora wa mwezi huo.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari na Mawasiliano wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), Kareem Boimada, Kikao cha Kamati ya Tuzo TFF, kilichokutana Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita, kilimchagua Feisal baada ya kuonyesha kiwango kizuri kwa Septemba na kutoa mchango mkubwa kwa klabu yake ikiwa ni pamoja na kufunga mabao mawili.

Alisema Feisal aliwashinda Moses Phiri wa Simba na Reliants Lusajo wa Namungo FC huku kwa upande wa Janza akiwashinda Charles Mkwassa wa Ruvu Shooting na Thierry Hitimana wa KMC FC.

"Kamati ya tuzo imemchagua Meneja wa Uwanja wa Majaliwa, Lindi kuwa meneja bora wa uwanja kwa mwezi Septemba kutokana na kufanya vizuri katika menejimenti ya matukio ya mchezo pamoja na masuala yanayohusu miundombinu uwanjani," alisema Boimada.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live