Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nabi agusia ishu ya Mukoko

Kaze Pic Mukoko Data Kiungo wa Yanga, Mukoko Tonombe

Sun, 31 Oct 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Nahodha msaidizi wa Yanga, Mukoko Tonombe amekuwa haonekani kwenye kikosi cha kwanza msimu huu hadi jana alipingia dakika za mwisho dhidi ya Azam na kocha wake ameeleza mambo ambayo yanachangia hilo na jinsi gani ataweza kurudi.

Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi amesema kuna mifumo miwili ambayo kama akipanga kutumia Mukoko ndio anaweza kuwemo kwenye kikosi cha kwanza au kuwa na kiwango bora zaidi ya sasa.

Nabi amesema kama akitumia mfumo wa 4-3-3, Mukoko anaweza kucheza katika eneo la viungo watatu ambapo watakuwa Yannick Bangala, Khalid Aucho pamoja naye.

Amesema mfumo mwingine 3-5-2, anaweza kuingia katika eneo la kiungo na atacheza chini zaidi katika ukabaji kutokana nyuma yake kutakuwa na mabeki watatu ambao muda mwingi atatakiwa kuwalinda.

“Jambo jingine unajua ni ngumu kwa kocha kufanya mabadiliko katika timu ambayo inampa ushindi kwenye mechi nyingi na hilo ndio lipo upande wangu. Kikosi cha sasa kinafanya vizuri,” amesema Nabi na kuongeza;

“Uwepo wa Mukoko unatoa uwanja mpana kwangu kama ikitokea Aucho au Bangala ambao wanacheza kwenye eneo ambalo analimudu mmoja akikosekana anakuwa mbadala sahihi.”

VIUNGO YANGA

Nabi alisema katika eneo la kiungo Yanga wapo Aucho, Bangala na Feisal Salum kulingana na viwango vyao ambayo wanaonyesha wakati huu inakuwa ngumu kwake kumuweka nje mmojawao katika kikosi cha kwanza bila sababu ya msingi.

“Mukoko anaweza kujituma zaidi ya alivyo wakati huu na akaonyesha kiwango bora katika mazoezi naye atapata nafasi ya kucheza kwani hilo ndio nahitaji katika timu,” amesema Nabi.

Kwa upande wa Mukoko alisema amekuwa akijitahidi kufanya mazoezi na kujituma kama vile ambavyo benchi la ufundi linahitaji na kuhusu kucheza au vinginevyo hilo si jukumu lake.

“Naamini katika uwezo wangu na nipo fiti na ikitokea nikapewa nafasi ya kucheza nitaonyesha kiwango kilichokuwa bora kama siku zote,” amesema Mukoko ambaye aliibeba sana Yanga msimu uliopita.

VIWANGO KULINGANA

Katika hatua nyingine Nabi amesema kwenye mazoezi ya wakati huu amekuwa akikomalia zaidi kuboresha kiwango kila cha mchezaji aliyekuwa benchi ili kilingane na wale wa kikosi cha kwanza.

Nabi amesema jambo hili na Mukoko kuonekana kuwa bora na hapati nafasi ya kucheza amepanga liwepo kwa wachezaji wote ili akimbadilisha mmoja na kuingia mwingine pasionekane upungufu na wote wanatakiwa kuwa sawa.

“Hata kama ikitokea kuna mchezaji atakosekana, anaumwa, kupewa adhabu, kupumzika nataka yule ambaye atakuwa ametokea benchi afanye kazi sawa bila timu kuonekana upungufu wowote,” amesema na kuongezea;

“Nimefanyia tathmini msimu uliopita, moja ya sababu ambazo zilitufanya kushindwa kufanya vizuri ni wachezaji waliocheza walikuwa hawalingani na wale waliokuwepo benchini.”

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz