KOCHA Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi amesema amelipanga upya jeshi lake ili kuhakikisha wanatoka na ushindi kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya KMC, akikiri wapinzani wao ni moja ya timu zenye ushindani na lazima wavaanae nao wakiwa na akili ya ziada.
Yanga imetua jana Songea tayari kuvaana na KMC kesho Uwanja wa Majimaji, ikiwa ni mchezo wa tatu baada ya awali kuzifumua Kagera Sugar na Geita Gold kwa bao 1-0 kila moja na Kocha Nabi alisema anawaheshimu wapinzani wao, lakini anataka kuendeleza moto.
“Sio mchezo mwepesi kwa kuwa kila timu itahitaji matokeo katika mchezo huo,” alisema.
“Tunatakiwa kupambana, hata vijana wangu nimeongea nao, kwani wapinzani wetu wameanza vibaya michezo miwili wamefungwa na kutoka sare, hivyo watapania nasi tunahitaji kujituma na kutoka na matokeo mazuri tena tukiwa ugenini.”
Nabi alisema ana imani kubwa na wachezaji wake katika kupambana japo hafurahishwi na idadi ndogo ya mabao wanayoyapata licha ya kucheza mpira vizuri.
“Nafanyia kazi kuhusu ufungaji, binafsi hata mimi japokuwa tunashinda ila idadi hiyo ya bao moja bado sijaridhika nataka tufunge zaidi na zaidi,” alisema.
Kocha msaidizi wa KMC, Habib Kondo alisema wapinzani wao wana uwezo na uzoefu mkubwa katika ligi, lakini anayejipanga ndiye anayeibuka na matokeo.
“Yanga nawaheshimu. Ni timu nzuri, hivyo mchezo utakuwa na ushindani kwa kuwa hata mimi nahitaji matokeo. Vijana wangu wanajua kila mchezo kwetu ni fainali hivyo inahitaji kupambana,” alisema Kondo.
WASIKIE WADAU
Mchezaji wa zamani wa Yanga, Akida Makunda alisema katika ligi hakuna timu ya kubeza, hivyo utakuwa mchezo mzuri kutokana na kila timu kuhitaji matokeo.
“Mwanzo wa ligi kila timu inajitahidi kujikusanyia pointi tatu muhimu. Hizi timu ambazo zilikuwa zinazungumzwa sana Simba na Yanga zinahitaji kuhakikisha zinapata matokeo, lakini pia namna ambavyo Yanga wamejiandaa kila mchezo fainali kwao KMC wanatakiwa kupambana,” alisema.
Tigana Lukinja, ambaye ni kocha kitaaluma alisema: “KMC uwanja wa Majimaji sio ambao wanautimia zaidi, hivyo yeyote anaweza kupata matokeo endapo ataheshimu mchezo,” alisema Lukinja.