Chati ya ufungaji Ligi Kuu Bara inaonyesha wanaoongoza kwa kupachika mabao ni viungo ambao wote walishawahi kucheza timu moja msimu uliopita (Yanga) chini ya kocha Nasredine Nabi ambaye amefichua jinsi walivyomtesa.
Mastaa hao wawili kila mmoja amefunga mabao mabao 13 mpaka sasa ikionekana ni vita ya kutafuta nani atakuwa mfungaji bora mwishoni mwa msimu.
Taarifa ziliwahi kusema kuwa sababu ya Feisal Salum kuondoka Yanga na kwenda Azam ni kumkimbia Aziz Ki, lakini sasa wanaonekana kupambana kila mmoja akiwa na kikosi cha timu yake.
Akizungumza na Mwanaspoti akiwa Morocco anakofundisha kikosi cha FAR Rabat kinachoongoza ligi, Nabi alisema mchuano wa viungo hao unadhihirisha ubora wa wawili hao aliokuwa anauona tangu awali.
Kocha huyo alisema kuwa mastaa hao ambao msimu uliopita alifanya nao kazi alipokuwa Yanga walikuwa ni miongoni mwa changamoto yake kubwa kwani ugumu ulikuwa namna ya kuwapanga na kuwatumia kwa wakati mmoja.
“Nafurahi kuwaona Feisal na Aziz wakichuana kwa ufungaji hii inadhihirisha wakati ule tulikuwa na watu bora sana eneo la kiungo na hata baada ya wao kuachana bado wameonyesha ubora huo, kila mmoja akiwa na timu yake ukweli walikuwa wakinitesa sana.
“Ngoja nikupe siri moja changamoto yangu kubwa wakati nikiwa Yanga ilikuwa ni matumizi ya Aziz KI na Feisal, hasa kama wote wako fiti na mechi inawahitaji, ilikuwa ili umuone Feisal anacheza sawasawa alitakiwa kucheza nyuma ya mshambuliaji wa mwisho.
“Azizi KI naye ilikuwa vivyohivyo, ilinipa homa kubwa kwangu kuamua kuna wakati nikapata akili ya kumtumia Aziz kucheza pembeni kidogo kwa nusu eneo ingawa alikuwa anajitahidi lakini niliona hana furaha na ilikuwa ngumu kumweka eneo hilo Feisal kwa kuwa alikuwa ametengeneza muunganiko mzuri na Fiston Mayele.”
Aidha Nabi aliongeza kuwa kuondoka kwa Feisal Yanga, kumempa nafasi kubwa Aziz Ki kuwa huru eneo hilo na sasa wote wanaonyesha makali yao wakiwa timu tofauti wakishindania ufungaji bora.
“Namjua Aziz sio mtu anayependa sana kufunga na kutengeneza nafasi lakini akicheza pale atawafunga sana kwani ana akili kubwa, vivyo hivyo kwa Feisal anajua kujiweka eneo zuri la kufunga, nadhani ni ushindani mzuri wanaoendelea kuuonyesha.
“Nadhani pia wananufaika na timu zote kukosa wale washambuliaji maalumu wanaojua kufunga mara kwa mara, wakati Feisal alivyokuwa Yanga alikuwa anafunga lakini hakuwa na nafasi ya kufunga zaidi ya Fiston, nadhani timu zote zinakosa wale washambuliaji sahihi wenye muendelezo mzuri wakufunga mabao,” alisema Nabi ambaye kwa sasa anakaribia kutwaa ubingwa wa Morocco.