Yanga Juzi imepata sare ya mabao 1-1, ugenini Mali dhidi ya Real Bamako kwenye mechi yake ya tatu ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi na sasa itarejea kujiandaa na mechi ya marudiano itakayopigwa Machi 9, mwaka huu uwanja wa Benjamin Mkapa huku ikirejea na somo kubwa juu ya mipira ya kutenga.
Mabingwa hao wa Kihistoria wa Ligi Kuu Tanzania Bara (28), katika mechi zao tatu za Kombe la Shirikisho Afrika wameruhusu bao kwenye kila mechi na mabao yote manne waliyofungwa yametokana na mipira ya kutenga jambo ambalo kocha mkuu wa timu hiyo, Nassredine Nabi amelistukia na sasa ataboresha eneo hilo.
Mabao hayo ni yale mawili ya US Monastir ugenini Tunisia ambapo la kwanza lilitokana na pigo huru 'Frikiki' na la pili likatokea kwenye kona.
Baada ya hapo bao lingine ililofungwa Yanga na TP Mazembe wakati Wanajangwani hao wakishinda 3-1 kwa Mkapa, lilifungwa kwa Frikiki ya moja kwa moja iliyovuka ukuta na kuzama nyavuni ikimshinda kipa Djigui Diarra. Bao lingine ni lile la juzi la kusawazisha kwa Real Bamako kwenye dakika za nyongeza ambalo lilitokana na mpira wa kona uliogongwa kichwa na kuingia golini na mechi kumalizika kwa matokeo ya 1-1.
Kocha Nabi amesema; "Nimeona aina hiyo ya mabao, siwezi kuwalaumu sana wachezaji wangu kwani mambo kama hayo kwenye mchezo yanatokea na najua inamuumiza kila mmoja wetu."
"Mara nyingi tumekuwa tukitafuta njia ya kuzuia mabao ya aina hii, ni jambo ambalo lipo kwenye muendelezo na tutaendelea kulifanyia kazi kuhakikisha linakoma kabisa na kutojirudia katika mechi zijazo."
Baadhi ya wadau walikuwa wanatoa maoni juu ya vimo vya mabeki wa Yanga kuwa vifupi wakiongozwa na Shomari Kibwana na Dickson Job lakini kauli yao imepingwa vikali na Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Yanga, Azam na Taifa Stars, Amri Kiemba anayeamini mipira ya juu shida sio kimo.
"Mipira ya namna hiyo wanalaumiwa sana mabeki kuwa wafupi lakini hiyo sio shida kubwa. Tatizo lipo kwenye namna ya kucheza mipira ya aina hiyo," alisema Kiemba ambaye kwa sasa ni Mchambuzi wa soka na kuongeza;
"Mipira ya juu mara nyingi inahitaji akili ya uharaka, makadirio na eneo, kama mchezaji atakuwa na hayo yote ataweza kucheza mipira a juu bila kujali mpinzani wake ni mrefu wa kiasi gani.
Tumeona mabeki wengi warefu wanashindwa kucheza kwa ufasaha mipira ya juu lakini wapo wafupi wanaoicheza vizuri hivyo Yanga inapaswa kulifanyia kazi mara kwa mara mazoezini na wachezaji kuzoea kucheza mipira ya aina hiyo."
Beki wa zamani wa Simba na Taifa Stars ambaye kwa sasa ni kocha mkuu wa timu ya taifa ya soka la ufukweni 'Beach Soccer' Boniphace Pawasa amesema tatizo la mipira ya kutenga sio kwa Yanga tu bali kwa miaka ya hivi karibuni limekuwa likilisumbua taifa kwa ujumla.
"Ni shida kwa taifa zima, kuna namna tunashindwa kucheza mipira ya kutenga kwa ujumla sio tu kuzuia hata kuitumia kupata mabao hivyo hatupaswi kuilaumu sana Yanga bali kutafuta njia," alisema Pawasa na kuongeza;
"Wachezaji wa Yanga wanatakiwa kuwa makini zaidi katika mipira hiyo hususani kwa aina ya wapinzani wanaokutana nao kimataifa, wengi ni wataalamu wa aina ya mipira hiyo hivyo kazi ya ziada inapaswa kufanyika."
Yanga inashika nafasi ya pili kwenye kundi D na alama nne nyuma ya Monastir inayoongoza na pointi saba huku TP Mazembe ikiwa nazo tatu nafasi ya tatu na Bamako ikiburuza mkia na mbili na timu zote zimecheza mechi tatu.