Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nabi: Walahi! Niachieni Yanga yangu

Yanga Picha Data Nabi: Walahi! Niachieni Yanga yangu

Sat, 25 Sep 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

KOCHA mkuu wa Yanga, Nasredine Nabi amesema mechi ya leo dhidi ya Simba itakuwa ngumu lakini wamejiandaa kushinda ili waanze msimu vizuri.

Alisema wamejipanga na wamefanya maandalizi mazuri tangu walipotolewa kwenye michuano ya kimataifa.

“Najua mashabiki hawakufurahishwa na kitendo cha kutolewa mapema kimataifa, hata sisi inatuuma sana, lakini tumejipanga kushinda mechi hii ya Simba kuwapooza. Tunajua wapo wengi sana. Tutapambana Mungu atusaidie kupata matokeo kwenye mechi hii,”alisema Kocha huyo.

Kuhusu upangaji wa kikosi alisema yeye ndio mpishi anajua kulingana na mazoezi wanayofanya na akaapa kabisa; “Walahi, hii Yanga ikiunganika mtakoma.”

Nabi aliyasema hayo wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuhusiana na mechi ya watani leo.

Nabi alisema kikosi chake kina wachezaji wazuri na bado kuna ushindani wa kutosha kutokana na uwepo wa nyota 28, huku kukiwa na sheria ya TFF ikiwataka wachezaji wa kigeni nane tu.

“Bosi GSM amefanya usajili mzuri tukishirikiana na kamati ya usajili na mimi nikiwepo, wachezaji hawa wakizoeana nina uhakika tutakuwa na timu nzuri,” alisema Nabi na kuongeza;

“Wachezaji majeruhi Yassin na Mapinduzi tayari wameanza mazoezi mepesi lakini hawatoweza kuingia moja kwa moja kwenye kikosi kwa sababu wana programu zao, wanahitaji muda kidogo.”

BOSI AWAITA NYOTA NYUMBANI

Ghalib Said (GSM) jana Ijumaa baada ya mazoezi kumalizika aliwaita nyota wote katika jumba lake la kifahari lililopo Kimbiji karibu na kambi ya Yanga iliyopo Avic Town.

Lengo kubwa la kuwaita wachezaji hao ilikuwa ni sehemu ya kuwapa maneno ya kuwaongezea morali wachezaji hao kabla hawajaingia kwenye mchezo wao wa leo.

Mwenyekiti wa klabu hiyo, Dk Mshindo Msola yeye alienda kutembelea mazoezi ya timu hiyo juzi Alhamisi jioni na jana kuwapa morali ya kwenye mchezo huo.

Endelea kufuatilia mitandao yetu ya kijamii tutakuwa LIVE Uwanjani siku nzima leo.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz