Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nabi: Simba? marufuku nawaambia...

Nabi Jukwaani Ll Makocha wa Yanga wakitazama mchezo

Mon, 28 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Juzi jioni Yanga ilikuwa uwanja wa nyumbani, Kwa Mkapa ikipambana na Mbeya City ambayo wiki iliyopita iliwashtua watani wao kwa kugawana nao pointi jijini Mbeya, lakini kuna mwongozo mpya wa kibabe wachezaji wa vinara hao wa Ligi Kuu Bara wamepewa na bosi wao, Nasreddine Nabi.

Nabi amewaambia hataki kusikia mchezaji anafuatilia na kuchekelea matokeo ya wapinzani wowote kwenye ligi wakiwemo Simba.

Kauli hii inawalenga mastaa wote wa Yanga wakiwemo vinara wao, Fiston Mayele anayeongoza kwa ufungaji wa mabao hadi sasa Ligi Kuu akiwa nayo manane, Faisal Salum ‘Feitoto’, Aziz Ki, Djigui Diarra na wengine akisisitiza anachotaka ni waangalie mechi zao na kila mchezaji ajipange kutumia mgawanyo wa nafasi za kucheza katika timu hiyo ili kuisaidia timu kushinda.

Amesema kufurahia matokeo mabaya ya wapinzani sio sahihi kwa sasa na hilo hataki kuona likizungumziwa.

“Sidhani kama ni sahihi kwa wachezaji au sisi makocha kuanza kuangalia na kufurahia matokeo ya timu pinzani kwetu, hii nimewaambia sitaki kuona mchezaji anazungumzia hilo au kujiona tumeshinda,” alisema na kuongeza;

“Kuna mambo ambayo tunatakiwa kuwaachia mashabiki wetu kufurahia ushindi wetu au matokeo mabaya ya timu zingine. Kila mchezaji wa timu hii anatakiwa kujipanga kwa kuangalia anapambanaje kuingia kwenye timu ya kwanza ili acheze aisaidie timu hii.”

Kocha huyo bora wa msimu uliopita wa ligi aliyechukua mataji matatu alisema ligi bado ndefu na lolote linaweza kutokea kwa kuwa mchezo wa soka yeyote anaweza kushinda.

“Nani alikuwa anajua Saudi Arabia inaweza kushinda mbele ya Argentina? Huu ndio mchezo wa soka wakati mwingine unashtua, ligi haijamalizika tena bado ndefu lolote linaweza kutokea.

“Tunachopaswa kufanya ni kuendelea kuhesabu kwa kushinda mechi zetu moja kwenda nyingine kisha tuangalie tumevuna ngapi mwisho wa msimu, hivyo ndivyo timu inayotaka ubingwa inatakiwa kuishi.”

Kocha huyo jana dhidi ya Mbeya City alifanya mabadiliko kadhaa eneo la kiungo akiendelea kutoa nafasi kwa wachezaji wake kuitumikia timu hiyo.

Chanzo: Mwanaspoti