Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nabi: Nililia kwa ajili ya Yanga na Rais Samia

IMG 4234 Nabi Kilioa.jpeg Nabi: Nililia kwa ajili ya Yanga na Rais Samia

Sat, 17 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mechi zipo mfululizo sana ligi ya hapa inachezwa wiki nzima, hakuna nafasi ya kutoa muda wa wachezaji kupumzika vizuri, nakubaliana na kwamba kuna wakati wiki moja ndani ya mwezi mkacheza katikati ya wiki lakini isiwe wiki zote ndani ya mwezi wachezaji wanaumia sana na sisi makocha tunakuwa katika wakati mgumu pia.

“Kuna wakati nilikumbana na adhabu ya kufungiwa hili nalo liliniumiza baadhi wa waamuzi nadhani wanatakiwa kujifunza lugha sio kila wakati mtu akiwa mkali kwako basi amekutolea lugha chafu, mimi ni mtu ninayejua kuwaheshimu wengine, sisi sote tunafanya kazi zinazotofautiana kidogo sio rahisi kwangu kumtukana mtu mwingine ni vigumu sana.

“Baadhi ya waamuzi wamekuwa wakifanya makosa yanayoumiza sana kuna vitu vya wazi sana walikuwa wanashindwa kuvitolea uamuzi unapolalamika anakutoa kwa kadi nyekundu wakati wote ambao waliniadhibu walinionea lakini nimewasamehe hakuna shida.

MECHI ZA MAKUNDI

“Tulipocheza mechi za hatua ya makundi hatukuanza vizuri tulitangulia kupoteza dhidi ya US Monastir, mechi ile iliniumiza kwa kuwa ile ndio timu ninayoipenda kutioka kwetu, nilitamani niwafunge ili kupeleka ujumbe kwao kuwa mtoto waliyenilea nimekuwa lakini haikuwa hivyo.

“Baada ya hapo tuliona mapungufu yetu tukabadilika na hata wachezaji waliazimia kubadilika kwenye mechi iliyofuatia dhidi ya TP Mazembe, tulibadilisha pia mifumo kutoka ule wa 4-2-3-1 na baadaye tukatumia 4-3-3 hapa ndipo tulianzia safari ya kushinda mechi zilizosalia, bahati mbaya sana tulipata sare ya ugenini kwenye mchezo ambao ilitakiwa tushinde.

Baada ya mechi za makundi kidogo tulibadilika na kuanza kuangalia mpango wa kucheza mechi kwa mechi lakini hapa tulitumia nguvu kubwa kwenye kuwachambua wapinzani ambao tulikuwa tunakutana nao, ilikuwa hatua nzuri kwa klabu kumleta Khalili (Ben Youssef) ambaye alifanya kazi kubwa tukishirikiana na sisi wengine ambaye alikuwa anatupa mwanga mkubwa wa kipi cha kufanya katika timu tulizokutana nazo.

HAKUSHANGAA YANGA KUTINGA FAINALI

"Tulipomaliza mechi za robo fainali na kisha nusu fainali siku shangaa kuona tunacheza fainali tayari kama kocha niliona kuna nafasi ya kucheza fainali lakini ilihitajika nguvu kubwa ya kuandaa timu ili hilo likamilike na kweli tukafika.

"Hapo nilianza kufikiria kwamba itakuwa vyema na heshima kwa klabu hii na Tanzania kwa ujumla tukichukua taji kwa kuwa hatukuwa kwenye eneo la kushindwa kupambana na USM Alger, kazi kubwa tuliifanya kuwandaa wachezaji kisaikolojia unajua sio wachezaji ambao waliwahi kufika ngazi hiyo kazi ambayo tuliona tumefanikiwa.

Bahati mbaya sana tukaanza kwa kupoteza nyumbani kwenye mchezo wa kwanza iliniuma sana kwa kuwa yalikuwa ni makosa yetu kwa kupoteza umakini na baada ya wapinzani wetu kutangulia niliona presha imewaingia wachezaji hata tuliposawazisha bado hawakuweza kutulia baadaye tukafanya kosa tena la kuruhusu bao la pili lile bao bado linaniuma mpaka leo pale ndipo tulipopoteza kombe, makosa yale hayakuwa rahisi kukubalika kwangu ukizingatia tulitumia nguvu kubwa kutafuta bao la kusawazisha.

"Hatukukata tamaa tulirudi kazini nikasema tubadilike kiukweli nilikuwa mkali kwa baadhi ya wachezaji lakini kwa nia njema ya kuwajenga kwa ajili ya mchezo wa pili, tulibadilisha mfumo na kutumia mfumo tofauti ambao sikuwahi kuutumia tangu nifike Yanga ambao ni 3-4-3, hili liliwapa tabu sana wapinzani wetu ingawa hata sisi ilitupa ugumu kwa wachezaji kuelewa na mwisho walicheza kwa ubora mkubwa.

"Kabla ya mchezo niliwaambia wachezaji waondoe presha na wala wasijali kama tutaruhusu goli twende tukatafute bao na mengine, tulipopata bao la kwanza niliona kama kuna nafasi kubwa ya sisi kuchukua kombe lakini yale ambayo wapinzani wetu waliyafanya kila mtu aliyaona haikuwa sawa yalitupunguzia nafasi ya kupata mabao mwisho niliumia kuona tumeshindwa kulipata kombe.

VURUGU ZA WAARABU ZILIWAPA UJASIRI WACHEZAJI

"Kabla ya mchezo tuliwaambia wachezaji zile vurugu tulizofanyiwa usiku na mashabiki wa USM Alger wazitumie kuwajenga kiujasiri na kweli wachezaji walipambana kama wanajeshi kwa muda wote wa dakika tisini. 

HII HAPA SIRI YA MACHOZI YAKE

"Nililia kweli, nilijikuta machozi nayanitoka, nitakupa siri mama yangu yuko Tunisia ni mzee sana lakini watu wanapaswa kujua kwamba hawezi kufuatilia sana mechi lakini alitaka anipe ratiba ya mechi za ligi ya hapa nyumbani na hata zile za mashindano mengine, kila siku ya kuamkia mechi huwa ametenga saa moja ya kuniombea dua na kuiombea Yanga ishinde ni mzee sana, huwa anaamka saa kumi alfajiri na kuniombea dua na timu kwa ujumla.

"Wakati nilipoongea naye kwamba tumefika fainali aliniambia maneno ambayo yananiuma mpaka sasa kwamba alisema mwanangu naomba chukua hili kombe kwahiyo nilipoona tumelikosa kombe nilijikuta nalia lakini sababu nyingine ni Yanga na Rais Samia, nilikwambia kabla kwamba nilishapanga mapema kuondoka niliona zawadi pekee ya kuwapa Yanga na Watanzania ni kuchukua kombe hili ambalo halijawahi kufika Tanzania.

"Mtu mwingine aliyeniumiza ni Rais Samia, ile hatua ya rais kutupa ndege na kuongeza morali kwa wachezaji nayo ilinipa maumivu, hii nchi inabahati sana kumpata rais kama huyu ambaye alipenda mafanikio niliwaambia hata wachezaji nendeni mkaipiganie nchi yenu nendeni mkampe faraja aliyewapa ndege hii ambayo imewaondolea uchovu mkubwa kama tungetumia ndege ya biashara, nawashukuru wachezaji walipambana sana lakini bahati haikuwa upande wetu.

ANAWEZAJE KUKAA MBALI NA FAMILIA?

Maisha ya Nabi yalikuwa yuko Tanzania lakini familia yake ipo Ubelgiji anakoishi hapa anaeleza jinsi maisha yalivyokuwa kwake akisema:"Ni vigumu sana haijawahi kuwa rahisi kwangu na hata kwa familia yangu, ndio maana nimekuwa kila ligi inaposimama kupisha mechi za timu ya taifa nami huwa nakimbia moja kuona familia mara moja.

"Ni maisha magumu sana lakini hakuna namna kwa kuwa mkewangu anafanya kazi kule ni vigumu kwambia aje huku sisi maisha yetu ni kuhamahama unaweza usiondoke lakini ukafukuzwa, watoto nao mmoja anafanya kazi (wakike) na huyu Hedi (wa kiume) naye anasoma chuo kwahiyo hakuna namna labda akipata likizo kama hivi anakuja mara moja kuniona hayo ndio yamekuwa maisha yangu, namshukuru sana mkewangu ni mker muelewa anayejua majukumu yake amekuwa anatekeleza majukumu makubwa ya kulea familia peke yake, ni mke bora sana kwangu.

YANGA IMEMFANYA MKEWE KUPENDA SOKA

"Kabla mimi kuja hapa mkewangu alikuwa hapendi soka, alikuwa anachukia kabisa wala hataki kuangalia mechi lakini nilipofika Yanga nikaona anaanza kufuatilia kila tunapocheza huku Tanzania na yeye anarudi nyumbani kufuatilia mechi kwa kuwa mara nyingi anakuwa amesharudi nyumbani nilikuwa nashangaa sana.

"Kuna wakati timu ikicheza ukiongea naye kwenye simu anajaribu kuanza kukuelezea makosa yalipofanyika unajua baada ya mimi kufika hapa na watu walivyokuwa wananipenda na wao famili wakaanza kuipenda zaidi Yanga.

HAPENDI MKEWE AWE UWANJANI WAKATI YANGA INACHEZA

"Tulipocheza fainali ya Kombe la Azam dhidi ya Coastal Union msimu mmoja uliopita, alikuwa hapa mkewangu alikuja na Hedi, lakini nilimzuia kuja uwanjani kwa kuwa huwa sipendi kumuona yuko uwanjani wakati wa mechi ngumu naona kama anateseka lakini Hedi alikuja.

"Tulipocheza na US Monastir kule Tunisia pia alikuja na Hedi kwa kuwa pale ni safari fupi alifika siku moja kabla ya mchezo tulizungumza nikamwambia kesho yake asubuhi arudi nyumbani akamuacha pia Hedi, sipendi kumuona anakuwa katika wakati mgumu kwasasabu ya mpira, mimi najua maumivu yake.

UONGOZI WA HERSI ANAUONAJE?

"Nilifanya kazi na Hersi katika sura mbili kwanza kabla ya kuwa Rais na baada ya kuwa Rais kusema ukweli huyu ni kijana ambaye ameyatoa maisha yake kwa ajili ya Yanga, nitawaambia sababu, kuna sajili ngumu ambazo zimefanyika hapa kama angekuwa ni ambaye hana mapenzi na Yanga asingehangaika lakini Hersi amekuwa kama mwanajeshi wakati wowote yuko tayari kuipigania Yanga.

"Hata baada ya kuwa rais maisha yake yamekuwa hayohayo, sisi tuliokuwa kwenye timu tunajua presha ya Hersi tunapokuwa tunakwenda kucheza mechi ngumu, kuna wakati anakuwa mkali kupitiliza lakini nilikuwa namuelewa kwa kuwa hata mimi hunitokea kuwa mkali kwa wachezaji pale ninapoona mambo hayaendi sawasawa.

"Sio Hersi peke yake na kamati yake ya utendaji angalia maisha ya Arafat (Haji makamu wa rais) naye ni mtu wa aina hiyohiyo ni watu wanaojituma bila kuchoka na wajumbe wao wa kamati ya utendaji, chini yao kuna Andre (Mtine Afisa mtendaji mkuu) naye ni mtu mwenye busara na aliyenyooka amekuwa msaada mkubwa kwangu.

"Naweza kusema huu ni uongozi ambao wanachama na mashabiki wa Yanga wanatakiwa kujivunia bahati nzuri wengi ni vijana hata kama watakuja kufanya makosa nani amekamilika chini ya jua? sisi sote tunaweza kufanya makosa jambo zuri kuna mazuri mengi wanafanya hebu angalia kwa umri wao mdogo wameiwezesha klabu kucheza fainali ya CAF kwangu ni uongozi ambao nitaukumbuka kwa wakati wote ambao nilifanya nao kazi.

"Pia nimshukuru Dk Msolla ambaye nilimkuta hapa na watu ambao pia niliwakuta walinipa ushirikiano mkubwa mpaka wanaondoka madarakani, alikuwa msaada kwangu alikuwa akiona kitu hakipo sawa anakufuata kesho yake na kukushauri.

"Kwenye klabu nyingi ambazo nimefundisha naweza kusema huu ni uongozi mzuri nadhani kama watampa ushirikiano kama huu kocha anayekuja basi Yanga itaendelea kufanya vizuri, kuondoka kwangu sitaki kuwa adui wa klabu hii na watu wake niko tayari kutoa ushirikiano wowote pale watakapohitaji mimi ni mwananchi kabisa

AWATOA WASIWASI MASHABIKI

"Najua mashabiki hawakufurahi kuondoka kwangu lakini nawaomba wanisamehe lakini niwaambie ni Nabi anandoka klabu kubwa kama hii wamepita makocha wengi lakini bado maisha ya mafanikio yalikuja, timu ipo bahati nzuri kila kinachotakiwa kuboreshwa kinajulikana hakutakuwa na shida kuendeleza mazuri haya ambayo nayaacha nyuma kwa jinsi ninavyoziona hesabu za viongozi wa Yanga naiona bado Yanga itaendelea kuwa klabu ya mataji zaidi.

Chanzo: Mwanaspoti