Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nabi Mpango umetiki, aikwepa Bamako

Nasreddine Nabi Tunis Nasreddine Nabi

Fri, 24 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Yanga iliilaza KMC 1-0 katika mechi ya Ligi Kuu juzi jioni na usiku wake ikapaa kwa ndege kuanza safari ya kuwafuata wapinzani wao Real Bamako ya Mali, lakini kuna salamu nzito kocha wa timu hiyo amezituma kuhusu wapinzani wao, akisema kazi inaendelea baada ya mipango kutiki.

Yanga imepaa kwa Ndege ya Shirika la Ethiopia ikiifuata Bamako kupitia nchini Ethiopia na kutua Mali jana mchana tayari kwa mchezo huo, huku ikiondoka na msafara wenye wachezaji 24 tayari kwa mchezo huo wa tatu wa Kundi D la michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Wakati Yanga ikipaa, kocha wake, Nasreddine Nabi ameliambia Mwanaspoti, hawataki kurudia makosa kama yaliyofanyika Tunisia walipoenda kucheza na US Monastir na kuchapwa mabao 2-0, kwa vile wanataka kuzipata pointi tatu za kwanza ugenini.

Yanga ilipata ushindi nyumbani katika mechi iliyopita ya CAF kwa kuichapa TP Mazembe ya DR Congo ukiwa ushindi wao wa kwanza, huku ikicheza pia soka kubwa na Nabi alisema wanaifuata Bamako ikiwa na mifumo mitatu ambayo wataamua ni upi wautumie huku akiringia kiwango walichoonyesha wakati wakiwapiga Mazembe.

Kocha huyo alisema dili lake la kutumia mfumo wa 4-3-3 ameridhishwa na jinsi safu yake ya kiungo na ile ya ushambuliaji ilivyopigana katika mchezo huo na kwamba kazi itaendelea hata kwenye mechi ya Jumapili hii ugenini mjini Bamako.

“Kitu bora tumetanua matumizi ya mifumo yetu na tunaweza kubadilika kulingana na mpinzani ambaye tutacheza naye kwa ubora wake, hii ni faida yetu kubwa,” alisema Nabi na kuongeza;

“Nimewaambia wachezaji, kuwa kitu ambacho kitatupa thamani kubwa ni kwenda kuendeleza ushindi wetu, ingawa nafahamu haitakuwa rahisi, tunapaswa kujitoa kwa kucheza kwa umakini mkubwa.”

Nabi aliongeza, ingawa bado anatamani kuona mambo makubwa zaidi lakini anafurahia muunganiko unaendelea kujitengeneza kwa washambuliaji wake wawili Fiston Mayele na Kennedy Musonda ambao kama kasi yao itazidi Yanga itashinda zaidi.

“Fiston na Musonda walicheza vizuri, tulikuwa tunataka nguvu ya namna hii, unaweza kuona Fiston hakufunga lakini kwangu mimi alifanya kazi kubwa kuutengeneza ushindi kwa kasi yake na pasi zake, hili likiongezeka zaidi tutakuwa na ubora wa kushinda zaidi.”

Kikosi cha Yanga kilichoondoka kimewajumuisha makipa Metacha Mnata, Eric Johola na Djigui Diarra, mabeki wakiwa ni; Ibrahim Hamad ‘Bacca’, Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, Mamadou Doumbia, Kibwana Shomari, Djuma Shaban, Joyce Lomalisa, David Bryson na Yannick Bangala

Wamo viungo Dickson Ambundo, Farid Mussa, Zawadi Mauya, Jesus Moloko, Khalid Aucho, Mudathir Yahya, Tuisila Kisinda, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, huku washambuliaji wakiwa Mayele, Musonda, Stephane Aziz KI, Clement Mzize.

Chanzo: Mwanaspoti