Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nabi: Mimi na Simba damdam

Nabi Mali 1024x1024 Nabi: Mimi na Simba damdam

Sat, 17 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Tuko sehemu ya mwisho ya mahojiano na aliyekuwa kocha wa Yanga Nasreddine Nabi hapa anaeleza kumbukumbu anayoondoka nayo ya mashabiki wa soka Tanzania akianza na wale wa Yanga akisema ni watu ambao watabaki kwenye kumbukumbu kubwa ya maisha yake.

"Naomba hapa unisikilize kwa umakini mimi naondoka lakini kama kuna watu watanirudisha Tanzania ni mashabiki wa soka wa Tanzania hasa nianze na hawa watu wangu wa Yanga, sijawahi kufanya kazi katika nchi yenye mashabiki wenye upendo kama hawa wa Yanga, sio tu sasa wakati naondoka lakini wakati wpte niliokuwa hapa walikuwa ni watu wa upendo mkubwa kwangu.

"Sikuwahi kupata shida nao waliishi kwa upendo mkubwa na mimi katika nyakati za huzuni na furaha, angalia wakati tunapoteza mechi bado wanakupigia makofi ya kukutia moyo hebu kumbuka mapokezi ya hivi karibuni tukiwa tunatoka Algeria, wapi utapata heshima kama ile? Tuposhinda pia wako pamoja na wewe kama kuna tuzo utaniambia niitoe ukiweka mbali ile ya Ghalib basi ya kwanza ni mashabiki wa Yanga.

HANA SHIDA NA SIMBA "Hata mashabiki wa wapinzani wetu Simba pia sikuwa na shida nao wakati wote ambao nimeishi hapa nao walikuwa marafiki zangu, ilikuwa nikikutana na shabiki wa Simba atanitania kwa haya majina ya utani ya Yanga Utopolo na mimi nitamjibu wewe kolo lakini mwisho tutafurahi na kupiga picha, ndio maana mnaona kila nilipopita sikuwahi kushindwa kuwasikiliza pale wanapotaka kupiga picha na mimi.

ATARUDI TANZANIA BAADAYE "Ndiyo, nitarudi Tanzania kama Yanga wataniambia nirudi siku moja huko mbele litakuwa ni suala la sekunde chache kukubaliana naondoka kwa wema sina shida na mtu kama yupo niliyewahi kumkosea anisamehe mimi ni binadamu, jambo zuri tumefanya kazi vizuri na hata klabu nimeiacha vizuri, niliwahi kuwaambia familia yangu napenda kuishi hapa, nitafikiria kujenga nyumba hapa lakini pia kujaribu kufanya biashara hapa ni sehemu salama kuishi.

"Sio lazima nirudi Yanga kama kocha naweza kurudi hata kwa nafasi nyingine ambayo klabu na mimi tutakubaliana, hii ni klabu ya maisha yangu kutokana na maisha mazuri niliyoishi na watu wake.

TAIFA STARS BAADAYE, MPENI MUDA AMROUCHE Nabi anasema timu ya taifa ya Tanzania ipo mikono salama chini ya rafiki yake kocha Adel Amrouche na kama atakuja kurudi Tanzania baadaye anaweza kuja kuifundisha endapo kocha huyo atakuwa ameondoka:"Kufundisha Tanzania inawezekana lakini labda baadaye sana tena kocha Adel (Amrouche) atakapoondoka.

"Adel ni kocha mkubwa sana pengine kuliko mimi namuheshimu sana nadhani Watanzania wakimpa muda kama ambavyo walinipa mimi watavuna mafanikio makubwa kutoka kwake ni kocha wa kisasa, wakati alipowaita wachezaji wa Yanga kwenye kikosi chake niliwaambia wakamsikilize kwa makini atawapa mafanikio.

MAYELE NI GOAL MACHINE "Ukiniuliza mchezaji wangu bora basi nitakutajia Fiston (Mayele) Yanga tulipata bahati kubwa kuwa na Mayele ni mchezaji mwenye kiu ya mafanikio na upendo ambao walimuonyesha watu wa Yanga ndio ulikuwa chachu kubwa ya kuipigania jezi ya klabu yake, kuna Mayele mmoja tu anafunga na kuipigania timu. "Kuna wakati zilikuja ofa za Fiston nilikuwa sehemu ya kuzuia asiuzwe kwa kuwa sio kila wakati utapata bahati ya kumpata mchezaji kama yeye sokoni, watu wajiulize ni lini walimkosa Fiston uwanjani?Jibu litakuwa rahisi ni pale alipoumia muda mwingi amekuw ana juhudi kuanzia mazoezini na hata kwenye mechi wapo wachezaji waliowahi kufikiria kudanganya wanaumwa ili wasicheze lakini sio Fiston.

"Kitu bora zaidi pia mashabiki wa Yanga pia walimpenda Fiston jina kubwa ambalo alikuja kulipata Tanzania sio rahisi kulipata sehemu nyingine, naamini bado anaweza kubaki Yanga lakini itategemea na uongozi utazungumza naye vipi, bado ana mkataba wa mwaka mmoja hapa.

MCHEZAJI ALIYEMSHANGAZA "Kama kuna mchezaji aliyenishangaza juu ya kipaji chake basi ni Dickson Job,wakati nafika na nilipoambiwa anacheza beki wa kati nilisubiri kuona ana kitu gani cha ziada lakini alinijibu kwa vitendo uwanjani, huyu ni kijana mdogo ambaye ana akili kubwa sana anapokuwa uwanjani, Job hajui kukataa jukumu unalomtuma amekuwa ni rahisi kwake kubadilika wakati wote kocha ukimtaka kufanya hivyo, ana nidhamu kubwa ni sawa na wale rafiki zake Kibwana (Shomari) na mwanangu Mshery (Aboutwalib) bahati mbaya aliumia lakini naye ni kipa mzuri, kwa Job ni bahati mbaya sana anacheza soka Tanzania.

HANA SHIDA NA MORRISON "Siku Morrison akiamua kucheza mpira hakuna mchezaji au winga mzuri kama huyu Afrika hii, lakini shida ni vutuko vyake, kuna wakati nilikasirika kumkosa uwanjani ka kuwa alikosekana wakati ambao timu inamuhitaji, shida yangu mimi na yeye ilikuwa moja tu hakutaka kufanya mazoezi sana ili awe tayari kucheza muda mrefu zaidi, ile kesi ya kukataa kutoka kwenye mechi pale uwanja wa Azam tulilimaliza tulimpa adhabu ya ndani sikuwa na shida naye tena,"alimaliza Nabi huku akicheka.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live