Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi amechukizwa na kitendo cha wachezaji wake kushindwa kuonyesha uwezo katika mchezo wao wa jana dhidi ya KMC kwa kile alichodai kuwa uwezo wao umekuwa duni na hawataki kubadilika.
Kocha Nabi jana alifanya mabadiliko makubwa ya kikosi chake akiwaondoa wachezaji nane wa kikosi cha kwanza na kuweka wachezaji wa kikosi cha pili kwenye mchezo huo.
Licha ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0, Nabi amesema kila mchezaji wa Yanga anapaswa kuipambania nembo ya timu yake, kuliko kubweteka na kukaa tu akiamini yupo Yanga timu kubwa.
"Hii mechi dhidi ya KMC, ni mechi mbaya sana katika mechi zote ambazo toka nimeanza kufundisha Yanga, wachezaji wanaweza kusema ni uchovu ila sio sababu ambayo wanaweza kutumia wachezaji wengine.
"Kwa sababu wachezaji wamesajiliwa ili kucheza, hata wale ambao walikuwa hawachezi nao ni wachezaji ambao wanapopata nafasi ya kuvaa jezi ya Yanga ni lazima waoneshe kitu ambacho walichonacho, unapewa nafasi unashindwa kuonesha.
"Kuna wengine toka miaka miwili wajiunge Yanga kiwango ni kile kile. Wachezaji wengine hawabadiliki, hawaoneshi tofauti na wakiwekwa nje wanasema mara fulani hachezi mara mwingine anacheza, wanaridhika tu kujiona wapo Yanga timu kubwa hawaangalii maisha yao ya baadae kisoka.
"Ndio maana mechi ya leo wachezaji waliopewa nafasi hawakutaka kujituma kwa kuonesha kile ambacho wanacho, wachezaji ambao wamepewa nafasi ya kuvaa jezi na hawakujituma wamenipa hasira sana," amesema Nasreddine Nabi.
KIKOSI CHA YANGA KILICHOANZA DHIDI YA KMC