Wakati Yanga ikibakiza saa chache kushuka Uwanja wa Olimpiki de Rades kupambana na wenyeji wao US Monastir kocha wa Yanga Nasreddine Nabi amesema timu yake hatatumia mbinu za kujilinda.
Nabi amesema Yanga haitatumia mifumo hiyo ya kujilinda lakini watakuwa na nidhamu kubwa ya kuzuia vizuri wakiwaheshimu wapinzani wao.
Kocha huyo ambaye ameweka rekodi ya kuwahi kuchukua pointi tatu katika ardhi ya Afrika ya Kaskazini akiwa na klabu kutoka Tanzania amesema anaamini wachezaji wake watashuka maelekezo yake katika mchezo wao wa kwanza wa hatua ya Makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
"Mimi sio muumini wa soka la kujilinda, tunataka kwanza kushinda hapa hilo ndio dhumuni letu kubwa, tutacheza kwa ubora wetu kama Yanga naamini wachezaji wanajua sasa cha kufanya baadaye," amesema Nabi
"Tumefanya kila lililondani ya uwezo wetu, viongozi wamekamilisha majukumu yao na sisi makocha tumemaliza majukumu yetu tulichobakiza ni wachezaji kuipigania klabu yetu.
"Ni mechi ngumu lakini mashabiki wetu hawatakuwa nasi hapa ila waiombee timu yao icheze kwa ubora tupate matokeo ya ndani ya malengo yetu."