Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi amesema wanafahamu makosa waliyoyafanya katika mchezo wa kwanza nyumbani dhidi ya Al Hilal ya Sudan na kulazimishwa sare ya 1-1, lakini akasema watakachoenda kukifanya ugenini jijini Khartoum, wenyeji hawataamini.
Nabi alisema hawataenda Sudan kinyonge kwani bado wana dakika 90 za kuamua matokeo ya kwenda makundi ama kuangukia kwenye play-off ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Akizungumza Nabi alisema kosa kubwa katika mchezo huo ni timu yake kushindwa kutumia nafasi ambazo walizitengeneza, japo anajivunia wachezaji wake jinsi walivyojituma katika dakika 55 za mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Kocha Nabi alisema hata hivyo licha ya matokeo hayo kuwaumiza mashabiki wao lakini bado kikosi chake kitashuka na utofauti mkubwa katika mchezo wa marudiano jijini Khartoum utakaopigwa wikiendi hii ili kuamua nafasi ya timu mojawapo kwenda makundi.
Alisema Yanga haitakwenda kinyonge jijini humo na wala hawatakwenda na mbinu za kujilinda katika mchezo huo ambao utapigwa Jumapili.
“Kuna sehemu tulifanya makosa sana ya kutotumia nafasi ambazo tulizitengeneza, tulicheza vizuri sana kipindi cha kwanza hasa dakika 55 za kwanza, tuliporuhusu goli hatukuonyesha ukomavu, tulinyon g’onyea sana,” alisema Nabi na kuongeza;
“Tunajua makosa yetu pia tunafahamu mashabiki wetu wameumia sana, huu ndio mchezo wa soka, hatujakata tamaa na wala hatutakwenda kurudiana nao tukiwa na akili ya kujilinda. Tutakwenda kuipigania Yanga, hii ni vita ya soka bado haijaisha tutazungumza na wachezaji kubadilisha muelekeo wa akili yao.”