Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nabi, Gamondi vita ya heshima na kisasi, tiketi zimeisha

Nabiii 0028 Gamondi na Nabi

Sun, 28 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Klabu ya Yanga itacheza mchezo wa mwisho wa kirafiki wa kimataifa leo Jumapili ambao ni wa kuwania Kombe la Toyota ikikutana na wenyeji, Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, lakini ikitarajiwa bato ya aina yake kwani inakikutanisha kikosi hicho dhidi ya kocha aliyekirejesha katika mstari misimu mitatu iliyopita.

Kaizer Chiefs maarufu kama Amakhosi, inafundishwa na Nasreddine Nabi aliyeipa Yanga mataji saba tofauti, ikiwamo mawili ya Ligi Kuu Bara, mawili Kombe la Shirikisho (FA) na Ngao ya Jamii mbili mbali na Kombe la Mapinduzi vilevile kisha akasepa zake Morocco.

Nabi baada ya kuondoka Yanga alitua FAR Rabat ya Morocco aliyoachana nayo mwisho wa msimu uliopita kisha kutua Amakhosi, waliokuwa wanamtaka kitambo hata kabla ya kuachana na Wa-nanchi.

Yanga itakuwa na mziki kamili kuelekea mchezo huo ikitaka kuweka rekodi ya kupata ushindi wa pili ndani ya ardhi ya Afrika Kusini.

Itakumbukwa katika ziara hiyo ilicheza na FC Augsburg ya Ujerumani na kuchapwa mabao 2-1 kisha kuwachapa wenyeji TS Galaxy kwa bao 1-0, mechi hizo mbili zikia maalumu kwa mashindano ya Kombe la Mpumalanga.

Yanga tangu iipe shida Mamelodi Sundwons ya huko huko Sauzi katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita, imejiwekea umaarufu mkubwa nchini humo ambapo leo itaangaliwa tena na maelfu ya mashabiki juu ya muendelezo wa kiwango.

Mabingwa hao wa Tanzania watakuwa pia na kiungo mshambuliaji, Pacome Zouzoua aliyekosa mechi mbili za kwanza baada ya kurejea kwao Ivory Coast kutengeneza pasi ya kusafiria.

Hata hivyo, mazoezi ya jana jioni ndio yaliyotegemewa kutoa picha kwa kiungo huyo kama atapewa muda gani wa kucheza au kukaa nje  kufuatia kukosa mazoezi ya wiki nzima ya timu yake.

Mbali na Pacome pia beki wao mpya wa kushoto Chadrack Boka naye juzi amefanya mazoezi ya kwanza na wenzake baada ya kupata maumivu kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya FC Augsburg kisha akakosa mechi ya Galaxy.

Akizungumzia mchezo huo, kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alisema, ingawa mchezo huo utakuwa na ubingwa kwa kutwaa taji kwa timu itakayoshinda, lakini hataki kutumia nguvu sana kwa kuwa bado wanaendelea kupandisha ubora na muunganiko wa kikosi chake.

“Tuna jukumu la kutengeneza kikosi kwa ajili ya msimu ujao, tutakuwa na mabadiliko mengi kwa kuwa bado tunaendelea kuwapima wachezaji wetu lakini kwa heshima ya timu yetu kama tukishinda litakuwa jambo linalopendeza,” alisema Gamondi, huku Nabi akisema kwamba bado anaendelea kuandaa kikosi kipya alichonacho ambacho hajasajili mchezaji yeyote hadi sasa, baada ya kambi ya Uturuki walikoweka kambi ya wiki mbili na nusu kumalizika na kurudia Sauzi.

Kocha huyo alipotua juzi nchini Afrika Kusini alipokewa kwa furaha na mamia ya mashabiki wa timu hiyo, lakini akawaambia wampe muda ili afanye kazi ya kuitengeneza Amakhosi mpya.

Nabi alisema kambi yao ya Uturuki ilikuwa na mafanikio kwa kuwa tayari anajua wachezaji gani watamsaidia na wapi wanahitaji kuongeza nguvu kuelekea msimu wake wa kwanza nchini Afrika Kusini.

“Tunakwenda kucheza na Yanga, naijua vizuri ni timu nzuri yenye kikosi ambacho hakina mabadiliko makubwa wakiwa na kocha mzuri,” alisema Nabi na kuongeza:

“Hatutaki kuweka akilini sana kuhusu ushindi, lakini kitu kizuri kwetu tunataka kuwaonyesha mashabiki wetu ni namna gani vijana wameanza kubadilika kutumia falsafa ninazotaka kuzitumia kwa muda nitakaokuwa hapa.

“Tunataka kucheza tofauti kidogo na soka walilozoea, tucheze mpira wa kuvutia na wenye kiu ya kutafuta ushindi, wachezaji wangu wakionyesha hili nitafurahi hata kama wakipoteza mchezo.

TIKETI ZIMEISHA

Saa chache baada ya kutangazwa mauzo ya tiketi za mchezo huo utakaofanyika Uwanja wa Toyota jijini Blomfontein zikamalizika fasta.

Uwanja huo unachukua mashabiki 46,000 waliokaa ndio utatumika kwa mchezo huo utakaoanza saa 9:00 kwa saa za Afrika Kusini lakini itakuwa saa 10:00 kwa saa za Afrika Mashariki.

Mbali na mchezo huo Amakhosi imewataka mashabiki hao kuwahi uwanjani ambapo kutakuwa na burudani mbalimbali za muziki na soka la wachezaji wao wa zamani.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live