KOCHA Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi amesema ushindi wa bao 1-0 walioupata dhidi ya Mbao FC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba ni hatua nzuri kuwania Kombe la Shirikisho la Azam ambalo msimu uliopita walipoteza katika mchezo wa fainali.
Yanga ilipata bao dakika ya 54 lililofungwa na Fiston Mayele akimalizia kwa kichwa mpira wa krosi iliyopigwa na Farid Musa.
Matokeo hayo yameifanya Yanga kufuzu hatua ya 16 ambapo sasa watakutana na Ruvu Shooting ambayo imetinga hatua hiyo baada ya kuiondoa KMC kwa mikwaju ya penalti 6-5 baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Akizungumza juzi baada ya mchezo huo, Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi alisema ulikuwa mchezo mgumu kwani Mbao ni timu nzuri na kuwashukuru wachezaji kwa kupambana na kuibuka na ushindi.
“Ni jambo zuri kupata ushindi inakupa nguvu kuingia kwenye mchezo unaofuata ukiwa na ari na akili yetu tunaihamishia katika mchezo unaofuata ambao naamini hautakuwa rahisi,” alisema Nabi.
Kocha wa Mbao FC, Ibrahim Mumba alisema ubora wa Yanga hasa safu ya ulinzi ulikuwa kikwazo kushindwa kutumia nafasi walizopata na kuwafanya kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo.
“Huu ulikuwa mchezo wetu muhimu kushinda katika mashindano ya Kombe la Shirikisho la Azam lakini tumeondolewa na sasa tunajipanga na michezo ya First League,” alisema Mumba.