Mashabiki wa soka wa Ufaransa hawakuwa na namna zaidi ya kutokwa tu na machozi baada ya kumwona N’Golo Kante akiwasili kujiunga na kikosi cha Les Bleus kwa ajili ya fainali ya Euro 2024 zitakazofanyika Ujerumani baadaye mwezi huu.
Kiungo huyo mkabaji aliitwa na kocha Didier Deschamps baada ya kukosekana kwenye kikosi cha timu ya taifa kwa kipindi cha miaka miwili.
Kante, 33, aliwasili kwenye kambi ya timu hiyo huko Clairefontaine akiwa kwenye mavazi ya kawaida sana pamoja na gari ya kawaida zaidi tofauti na ambazo mashabiki wamezoea kuziona zikiendeeshwa na mastaa wengine wa Les Blues.
Kama kawaida, Kante alishuka kwenye gari yake na kuonyesha tabasamu pana akiwa hana shaka yoyote, kitu ambacho kiliwapa hisia kali mashabiki kwa namna mchezaji huyo asivyojivuna.
Baada ya hapo, gumzo lilihamia kwenye mitandao ya kijamii, ambako shabiki mmoja alisema: “Bado nampenda huyu mtu, namfikiria vile anavyopora watu mipira. Jamaa ni mtulivu.”
Shabiki wa pilia alisema: “Nilifurahi kumwona akitasabamu tena, nilimmisi sana huyu jamaa.”
Shabiki wa tatu aliandika: “Huwezi kuwa na sababu ya kumchukia Kante.”
Mwingine aliongeza: “Nampenda sana, ananifanya nitake kulia.”
Kante kwa sasa anakipiga huko Saudi Arabia kwenye kikosi cha Al-Ittihad, ambapo anacheza na mastaa wengine matata kabisa akiwamo Karim Benzema, Jota, Fabinho na Luiz Felipe.