Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mzuka wa Anfield na Arne Slot

Arne Slot Kocha, Arne Slot

Mon, 27 May 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Juni 1, Liverpool itafunga zama za Jurgen Klopp na kufungua zama mpya za Arne Slot.

Kocha huyo wa Feyenoord, Slot, hataki kutumia muda mrefu kabla ya kwenda kuanzisha zama zake huko Anfield.

Mdachi huyo anataka awe na kikosi chake tangu mwanzo wa ‘pre-season’ ili kukifuma kianze kucheza kwa mtindo wake. Bila shaka Liverpool itakaribisha sura mpya kwenye kikosi kwa ajili ya kocha huyo, lakini kutakuwa na mastaa wengine watakaofunguliwa mlango wa kutokea.

Joel Matip na Thiago Alcantara wataondoka mikataba yao itakapofika tamati mwisho wa msimu, hivyo kutahitajika mastaa wengine wa kwenda kwenye kikosi hicho kuziba mapengo.

Kocha Slot, atahitaji kukaa kitako na mabosi wanaohusika na usajili, Michael Edwards na Richard Hughes kujadili ni mchezaji gani wa kuingia kwenye kikosi.

Mfumo wa kiuchezaji unaopendelewa na kocha Slot ni 4-2-3-1, ukitofautiana na ule wa Klopp wa 4-3-3. Slot, 45, atakuwa na mambo kadhaa ya kuamua kwenye dirisha hili la kwanza kwake akiwa na Liverpool. Trent Alexander-Arnold, Virgil van Dijk na Mohamed Salah wote wataingia kwenye miaka ya mwisho kwenye mikataba, hivyo ni suala kubwa juu ya nani atabaki, nani ataondoka. Na vyovyote itakavyokuwa, hii Liverpool itakavyokuwa kwa kuanzia chini ya Slot.

-Kipa na mabeki; Licha ya Alisson kutetereka kiasi na kumfanya Caoimhin Kelleher kupata nafasi ya kucheza, hilo halina maana kwamba Mbrazili huyo ataondoka majira hayo. Mbele ya kipa, Alisson, moja ya mabeki wa Feyenoord anayehusishwa na Liverpool, Lutsharel Geertruida, huenda akanaswa na kutua Anfield. Kocha Slot atakuwa na kitu cha kufikiria pia kwa mabeki wa pembeni, Andy Robertson na Joe Gomez wanaweza kutumika vyema, huku nafasi nyingine ya beki wa kati, itategemea na Van Dijk kama atabaki, la Jarell Quansah atapewa nafasi.

-Kiungo; Alexander-Arnold ana uwezo wa kucheza beki ya pembeni, lakini kwenye mfumo unaochezwa huko Feyenoord, kocha Slot, Mwingereza huyo atacheza kwenye sehemu ya kiungo.

Alexis Mac Allister ni mchezaji mwingine anayehusishwa na Real Madrid, licha ya kwamba hana haraka ya kuondoka Anfield. Ni chaguo jingine zuri la kiungo ya kukaba katikati ya uwanja.

Staa mwingine wa kuongezwa kwenye kiungo ni Teun Koopmeiners. Mdachi huyo amekuwa kwenye rada za Liverpool kwa muda mrefu, hivyo kitendo cha timu sasa kuwa chini ya kocha Mdachi, kinaweza kumvutia mkali huyo wa Atalanta.

Kwenye Namba 10, Slot atakuwa na machaguo ya kufanya, aanze na Dominik Szoboszlai au Harvey Elliott. Eneo hilo la kiungo kwa wachezaji waliopo Liverpool, bado lipo salama sana.

-Washambuliaji; Swali kubwa linaloulizwa hapa ni kuhusu hatima ya Mo Salah. Kama ofa kubwa italetwa kutoka kwa klabu za Saudi Arabia kuna wasiwasi staa huyo wa Misri akaondoka. Lakini, kwa ilivyo sasa, atabaki na atacheza kwenye upande wa kushoto, huku Luis Diaz, anayehusishwa na Paris Saint-Germain, akibaki Anfield, atapangwa kwenye upande wa kulia.

Diogo Jota atasimama kwenye nafasi ya mshambuliaji wa kati na hapo atakuwa anabadilishana na Darwin Nunez, kama hataenda Barcelona huku mwingine kwenye nafasi hiyo ni Cody Gakpo.

Chanzo: Mwanaspoti