Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mzizima derby...Kaze atangaza vita

Kaze Pic Cedrick Kaze

Fri, 23 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedrick Kaze amefurahishwa na kiwango kilichoonyeshwa na mastaa wake kwenye mchezo dhidi ya Coastal Union akisema ni chachu ya kuendeleza ushindi kwenye mchezo dhidi ya Azam FC, Jumapili.

Yanga juzi iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Coastal Union kwenye Ligi Kuu uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar. Mechi kati ya Azam na Yanga ambayo hufahamika kama Mzizima Derby imekuwa ikisubiriwa kwa hamu na mashabiki wa timu zote kutokana na ubora wa timu hizo.

Katika mchezo wa kwanza ulipigwa kwenye Kwa Mkapa timu hizo zilitoshana nguvu kwa sare ya mabao 2-2, jambo ambalo linaongeza ushindani kwenye mchezo huo. Kaze alisema wachezaji wake walifanya kazi waliyoelekezwa, benchi la ufundi wamechukua hatua za haraka kuwakimbiza mastaa hao ‘gym’ ili kuweka miili yao kwenye utimamu mzuri wa mwili kutokana na kuwa na mechi ngumu mbele.

“Kila mchezaji ameonyesha jitihada zake binafsi leo ‘jana’ tulianza na mazoezi mepesi na baadaye gym malengo ni kuweka miili sawa hii kuwasaidia kuwafanya wachezaji wajisikie vizuri na kuiweka sawa miili yao,” alisema na kuongeza;

“Tunatarajia mchezo mgumu na wa ushindani kwa sababu Azam FC ni miongoni mwa timu ambazo zinatufuata kwa pointi hatutarajii kuangusha pointi hata moja ili tujiimarishe kileleni hadi tunatetea taji.”

Kaze alisema wanawaheshimu wapinzani wao na wao wamejiandaa kwa ajili ya kushindana ili kuweza kufikia malengo waliyokusudia wanatambua ubora wa Azam FC na wao ni bora.

Yanga imeendelea kuonyesha ubora msimu huu ukiwa na pointi 44 baada ya kucheza michezo 17 ikiwa imetoka sare michezo miwili dhidi ya Simba na Azam na kupoteza mmoja dhidi ya Ihefu, hata hivyo inakutana na Azam ambayo kabla ya mchezo wa jana ilikuwa haijapoteza kwenye michezo minane ikiwa nafasi ya tatu na pointi 36, baada ya kutoka sare mara tatu na kupoteza michezo miwili.

HATMA YA NKANE LEO

Mchezaji wa Yanga, Denis Nkane amefunguka kuhusu hali yake.

“Siyo nzuri nilipata matatizo kwasababu niliruka juu zaidi ya kimo changu na kudondoka ninachofahamu hadi sasa ni nyama za paja zimechanika japo nasikia maumivu makali kwa ndani. Nahisi kuna kitu kingine, acha tusubiri majibu,” alisema Nkane ambaye aliumia vibaya kwenye mchezo wa juzi dhidi ya Coastal Union.

“Vipimo vimefanyika lakini nimeambiwa majibu ya MRI yatatoka kesho (leo), hivyo naomba Mungu yasiwe ya kuniweka nje kwa muda mrefu kwa sababu bado nahitaji kupata nafasi ya kucheza kutokana na ushindani wa namba uliopo ndani ya timu.”

Chanzo: Mwanaspoti