Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mzize awaibua mafaza Simba, Yanga

Clement Mzize X Maxi Mpia Nzengeli Mzize awaibua mafaza Simba, Yanga

Mon, 13 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kazi kubwa iliyofanywa na Clement Mzize kwenye pambano la watani, Simba na Yanga lililopigwa Novemba 5 na Mnyama kulala kwa mabao 5-1 imewaibua wakongwe waliowahi kutamba na timu hizo na kumtaka nyota huyo chipukizi aendelee kuaminiwa.

Jina la Mzize limetajwa kutokana na kuungana na wakali wengine walioamua matokeo ya mechi za klabu hizo kongwe hasa wale waliokuwa wakifunga mabao ya jioni na kuziokoa timu hizo kufungwa ama kwa kutoka sare kama sio kushinda.

Ipo hivi. Wapo mastaa Simba na Yanga, waliamua matokeo ya ushindi kwa baadhi ya mechi ambazo timu hizo zimecheza, vinginevyo zingefungwa, kuambulia sare ama suluhu.

Mwanaspoti linakuchambulia mastaa hao ambao mabao ya mwisho yalizivusha timu zao kupata matokeo ya ushindi na kuwapa furaha mashabiki wao.

YANGA 1-0 NAMUNGO

Mchezo huo ulipigwa Uwanja wa Azam Complex, Septemba 20 dakika ya 88 kiungo wa Yanga, Mudathir Yahya aliwanyanyua mashabiki baada ya kufunga bao na timu yake kupata pointi tatu, mechi ilikuwa ngumu na ya ushindani mkali.

COASTAL UNION 0-1 YANGA

Baada ya Yanga kutoka kuichapa Simba mabao 5-1, mchezo uliofuata ulikuwa dhidi ya Coastal Union, uliopigwa Uwanja wa Mkwakwani, Novemba 8, haukuwa rahisi kwa upande wao. Mchezaji aliyeokoa jahazi la kujinyakulia pointi tatu ni Mzize aliyefunga bao dakika ya 71 akitokea benchi.

YANGA 3-2 AZAM FC

Mchezo huo ambao ulipigwa kwenye Benjamin Mkapa, Oktoba 23 na kumalizika kwa mabao 3-2, staa wa Yanga Aziz Ki ndiye aliyeibeba klabu yake akifunga hat-trick kwenye mechi ambayo ilikuwa na ushindani mkali.

SIMBA 1-1 NAMUNGO

Straika wa Namungo FC, Reliants Lusajo ndiye alikuwa wa kwanza kuipa timu yake bao dakika 29 lililodumu hadi kipindi cha pili dakika ya 75, Jean Baleke akifunga na kufanya timu yake iambulie pointi moja, mchezo huo umepigwa Uwanja wa Uhuru, Novemba 9.

SINGIDA BIG STARS 1-2 SIMBA

Mechi hiyo ilipigwa Oktoba 8, Uwanja wa Liti mkoani Singida, mchezo ulikuwa mgumu na mashabiki wa Simba ni kama walitaka kukubaliana na sare, Moses Phiri ndiye aliyeipa pointi tatu timu yake baada ya kufunga bao la pili dakika 83.

KWA MZIZE SASA

Kwenye mechi dhidi ya Simba ilionekana kuibana Yanga na kwenda mapumziko zikiwa nguvu sawa kwa kufunga bao 1-1, lakini Kocha Miguel Gamondi wa Yanga alimtoa mfungaji wa bao la timu hiyo, Kennedy Musonda na kumuingia Mzize aliyeubadili mchezo na Simba kulala 5-1.

Mbali na kuasisti, lakini Mzize kwenye mechi ya katikati ya wiki ya mwisho kwa Yanga ugenini dhidi ya Coastal Union, mchezaji huyo aliingia kutoka benchi na kufunga bao pekee lililoipa timu hiyo pointi tatu muhimu, jambo lililowaibua wachezaji wakongwe wa soka nchini akiwamo Mohamed Banka aliyesema kwa ukubwa wa klabu hizo, zinatakiwa kuwepo na mastaa ambao wanaamua matokeo kwenye michezo migumu.

“Mfano mzuri Mzize ni mzawa aliyepandishwa kikosi B cha Yanga, baadhi ya mechi tangu msimu uliopita aliamua matokeo na ni mzawa ambaye anaweza akaisaidia hata Stars, hivyo kwa ukubwa wa na ukongwe wa klabu hizo, zinatakiwa ziwe na mastaa wenye kufanya maamuzi penye ugumu,”alisema.

Hoja yake iliungwa mkono na staa wa zamani wa Yanga, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ aliyesema: “Yanga na Simba ni klabu kubwa, zinazolipa vizuri wachezaji wake, hivyo lazima ziwe na mastaa wa kuamua mechi ngumu na kama zinakosa watu wa aina hiyo, zinapaswa kujitafakari zaidi, kwani nje na Ligi Kuu zinapata nafasi ya kucheza michuano ya CAF.”

Mzize ndiye aliyeivusha Yanga kuingia makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya timu hiyo kusota kwa miaka 25 tangu ilipocheza mara ya kwanza mwaka 1998 kwa mabao mawili aliyoitungua Al Merrikh ya Sudan nje ndani katika mechi za raundi ya pili.

Alifunga wakati Al Merrikh iliyokuwa haijawahi kufungwa au kung’olewa na Yanga michuanoni ilipoilaza 2-0 jijini Kigali, Rwanda kabla ya kuzima tena waliporudiana jijini Dar es Salaam.

Chanzo: Mwanaspoti